Mahakama Kuu Kanda ya Iringa iliyofanya kikao chake mkoani Njombe, imemuhukumu Joel Nziku kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua watoto watatu wa familia moja ambao ni watoto wa baba yake mdogo.

Nziku alitekeleza mauaji hayo mwezi Januari mwaka 2019 katika kijiji cha Ikando kata ya Kichiwa katika halmashauri ya wilaya ya Njombe.
Imedaiwa kuwa mshitakiwa alikwenda nyumbani kwa baba yake mdogo na kuwachukua watoto watatu ambao aliwapakia kwenye lori ambapo aliwaua kwa kuwapiga na kitu kizito na baadaye kwenda kuitelekeza miili yao katika maeneo tofauti.
Mshitakiwa alikuwa na mgogoro na baba yake mdogo Danford Nziku, ambaye ndiye baba wa watoto watatu waliouawa ambao ni Giliad Nziku, Gaspa Nziku na Godliver Nziku.
Pamoja na mshtakiwa kukana kuhusika na mauaji pamoja na kukana kutowafahamu watoto waliouawa, Mahakama imesema kupitia vielelezo na mashahidi tisa walioapa na kutoa ushahidi mahakamani, mahakama imemkuta mshitakiwa na hatia.