Jitihada za Kumpata,Kumuoka Rais wa Iran Zinaendelea

Vikosi vya ukoaji nchini Iran vinaendelea na jitihada za uokoaji katika ajali ya helikopta iliyombeba Rais wa Iran Ebrahim Raisi na wanasiasa wengine wa ngazi za juu,kulingana na televisheni ya taifa ya Iran, timu za waokoaji zinatajwa kuyafikia mabaki ya helikopta iliyokuwa imembeba Rais wa Iran Ebrahim Raisi na Maaafisa wengine. 

Televisheni ya taifa ya Iran imeripoti kuwa hakuna dalili ya mtu aliye hai katika eneo la ajali,wakati mkuu wa shirika la Hilali Nyekundu la Irani Pirhossein Koolivand amesema helikopta hiyo imepatikana na kwamba timu za uokoaji zilikuwa zikisogea karibu na eneo la ajali akiongeza kuwa kuwa hali si nzuri.

Helikopta hiyo iliyombeba Raisi, ilianguka katika eneo la mbali kaskazini mwa Iran Jumapili jioni kutokana na hali mbaya ya hewa ambayo pia imetajwa kutatiza shughuli za uokoaji katika kipindi ambacho hadi kufikia asubuhi ya Jumatatu ya Leo yamepita zaidi ya masaa 12 tangu ajali hiyo ilipotokea na Rais wa Taifa hilo kutojulikana aliko.

Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kwamba waliokua safarini na rais katika helikopta hiyo ni waziri wa mambo ya nje wa Iran Hussein Amirabdollahian, Gavana wa jimbo la Azerbaijan Mashariki Malek Rahmati na abiria wengine kadhaa Aidha kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Iran, helikopita hiyo imepata ajali karibu na eneo la Jolfa, zaidi ya kilomita 600 kutoka Tehran karibu na mpaka na Azerbaijan.

Nchi kadhaa zikiwemo Urusi na Uturuki zimetoa msaada katika operesheni ya uokoaji, huku ndege isiyo na rubani ya Uturuki pia ikiruka katika anga ya Iran kusaidia shughuli ya utafutaji na kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amewatolea mwito Wairan kumwombea Raisi.

Baadhi ya raia wa Iran Wakifanya Maombi kwaajili ya Rais wa Taifa hilo Ebrahim Rais aliyepata ajali ya Helikopta Jumapili ya Mei 19,2024.

Ebrahim Raisi aliyezaliwa mwaka 1960 huko Mashhad Kaskazini Mashariki mwa Iran aliapishwa kama rais mpya wa Iran mnamo Agosti 2021 baada ya kushinda  uchaguzi wa urais mwezi Juni na chini ya asilimia 62 ya kura kama mgombea mkuu wa vyama vya siasa kali na anayependwa zaidi na mwenye ushawishi mkubwa ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislam akidumisha uhusiano wa karibu na Khamenei.

Kwa mujibu wa katiba, Raisi ni kiongozi nambari mbili nchini Iran, akimfuata Khamenei aliye mkuu wa nchi na pia ndiye mwenye uamuzi wa mwisho katika masuala yote ya kimkakati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *