JESHI LA POLISI SHINYANGA LAKAMATA DHAHABU FEKI NA GOBORE…

 NA EUNICE KANUMBA – SHINYANGA

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi amesema kuwa Jeshi la Polisi Shinyanga, limefanikiwa kukamata madini ya dhahabu bandia gramu 250, wamekamata jumla ya watu 81, bangi gramu 9,000, mirungi bunda tisa, gongo lita 113, sola panel saba, betri nne za sola, pikipiki 11, kadi tatu za pikipiki, antena nne za ving’amuzi.

Vingine ambavyo Jeshi la Polisi limekamata ni redio mbili, baiskeli mbili, mashine moja ya bonanza, kamera moja na mitambo minne ya kutengeneza gongo. “Katika msako huu tumefanikiwa pia kukamata silaha aina ya gobore kwenye kijiji cha Bugomba A Ushetu wilayani Kahama, mtuhumiwa alikuwa ameibeba kwenye baiskeli na alipoona gari la Polisi alikimbia na kuitelekeza bado tunamsaka,” – RPC Magomi.

Kamanda Magomi pia ametangaza mafanikio ya kesi mahakamani, ambapo jumla ya kesi 18 zimepata mafanikio, na washitakiwa wameshapatikana na adhabu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kifungo cha maisha jela kwa washitakiwa wanne wa unyang’anyi wa kutumia silaha.

 Aidha, kesi nyingine zimehusisha makosa ya kubaka, kumlawiti, kumiliki nyara za serikali kinyume na sheria, dawa za kulevya, wizi, na uvunjaji wa nyumba, ambapo washitakiwa wamehukumiwa kifungo cha kati ya miezi mitatu hadi miaka 30 jela.

Kwa upande wa operesheni za usalama barabarani, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kukamata jumla ya makosa 5,376, ambapo makosa ya magari yalikuwa 3,767 na makosa ya bajaji na pikipiki yalikuwa 1,609. 

Wahusika walilipa faini za papo kwa hapo. 

Jeshi la Polisi pia limeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu kupinga ukatili wa kijinsia, ulinzi shirikishi, na usalama barabarani, na limezindua kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *