Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu
Hassan ameliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha linaimarisha maadili kwa vitendo kwa Maafisa na Askari wake, ili kulinda heshima ya taasisi hiyo na kuzidi kujenga imani ya Wananchi kwa vyombo vya dola.
Rais Dkt. Samia ametoa agizo hilo hii leo Juni 9, 2025 katika sherehe za kufunga Mafunzo ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi Na. 1 ya Mwaka 2024/2025 katika Chuo cha Taaluma ya Polisi (DPA) Kurasini jijini Dar es Salaam ambapo jumla ya wahitimu 955 walitunukiwa vyeti baada ya
kuhitimu mafunzo yao ya miezi tisa.

Aidha, Rais Dkt. Samia amesema mafanikio ya Jeshi la Polisi katika kulinda raia na mali zao hayawezi kupatikana endapo maadili yataendelea kudorora miongoni mwa watendaji wake, huku akisisitiza kuwa nidhamu, uadilifu na uaminifu kwa umma ni msingi imara wa kuijenga taasisi ya Polisi inayoaminika na kuheshimiwa na wananchi.
Hali kadhalika, Rais Dkt. Samia amewataka wahitimu hao kuzingatia viapo vyao vya kazi,
kuepuka vitendo vya rushwa na kuwa kielelezo cha mabadiliko chanya na maboresho ya kiutendaji kwenye maeneo yao ya kazi.

Akizungumzia usalama barabarani, Rais Dkt. Samia ameliagiza Jeshi la Polisi kuimarisha
mikakati ya kudhibiti ajali za barabarani, akisema licha ya kushuka kwa jumla ya idadi ya ajali na vifo katika mwaka mmoja uliopita, bado takwimu za vifo ni kubwa.
Rais Dkt. Samia pia amelitaka Jeshi la Polisi kuongeza ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kudhibiti ajali hizo kwa ufanisi zaidi.


