Jeshi la polisi katika mkoa wa Mwanza linamshilikilia Doto Maduhu mkazi wa Kishiri, wilaya ya Nyamagana kwa tuhuma za kumbaka, kumlawiti na kumshambulia mtoto wa kambo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kumi ambae jina lake limehifadhiwa.
Akizungumzia tukio hilo kamanda wa jeshi la polisi katika mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa amesema jeshi la polisi lilipokea taarifa kutoka kwa raia mwema kua mtoto huyo alikuwa anafanyiwa ukatili huo mara kwa mara na kusababisha hali ya kiafya ya mtoto kuwa dhaifu ambapo kutokana na taarifa hizo jeshi la polisi lilifika katika eneo hilo na kumkuta mtuhumiwa huyo akishirikiana na mke wake aitwae Aneth Sijaona wakifanya jitihada za kumpeleka mtoto huyo hospitali ili apate matibabu na walifika katika kituo cha afya cha Usumau kilichopo eneo la Kishiri ambapo walielekezwa kumpeleka mtoto huyo katika Zahanati ya serikali Igoma ndipo katika harakati za matibabu mtoto huyo alifariki dunia tarehe 30.12.2024
majira ya saa nne usiku.
Katika hatua nyingine Mutafungwa pia amesema jeshi la polisi pia linamshikilia na kuendelea kumhoji mama mzazi wa mtoto huyo aitwaye Aneth Sijaona Mhano kwa kushindwa kutoa taarifa kwa Jeshi la polisi au kwa jirani zake juu ya ukatili aliokuwa akifanyiwa mtoto ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa na kuokoa maisha ya mtoto huyo.
Aidha pia amesema Mwili wa mtoto huyo umefanyiwa uchunguzi na madaktari na tayari umekabidhiwa kwa baba mzazi wa mtoto huyo aitwaye Emmanuel Daud, miaka 28, dereva na mkazi wa Maduka tisa, wilaya ya ilemela na ndugu wengine kwa ajili ya mazishi.
Kufuatia tukio hilo Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza linawakumbusha wananchi hususani wazazi na walezi kuchukuwa tahadhari na kuzingatia malezi bora ya watoto ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili pia linawakumbusha kuwa vitendo vya ukatili kwa watoto hufanywa na watu walio karibu na watoto kwa misingi ya undugu, malezi na ujirani huku pia likiwaomba wananchi kuendelea kutembelea madawati ya jinsia na watoto yaliyopo kwenye vituo vya polisi kwa ajili ya kutoa taaarifa kuhusu matukio yote ya ukatili wa kijinsia.