Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza limemkamata kwa mahojiano Diana Edward Bundala (42), ambaye ni maarufu kwa jina la Mfalme Zumaridi, kutokana na tuhuma za kuyageuza makazi yake kuwa kanisa na kuendesha shughuli za kidini.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza hii leo Mei 15, 2025 imeeleza kuwa Zumaridi alikamatwa majira ya saa nne asubuhi katika mtaa wa Buguku, uliopo kata ya Buhongwa, wilaya ya Nyamagana.
“Mfalme Zumaridi, mkazi wa mtaa wa Buguku, kata ya Buhongwa, ambaye bila usajili pamoja na kufanya mahubiri kwa waumini wake kwa sauti ya juu katika eneo hilo ambalo ni makazi ya watu na kusababisha usumbufu kwa majirani wanaoishi karibu na makazi yake,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, Zumaridi pia anahojiwa kuhusiana na taarifa inayoendelea kusambaa katika
mitandao ya kijamii akionekana kwenye picha mjongeo akiwa na kundi la watoto wenye umri mdogo wa jinsia ya kike na kiume akiwaeleza kuwa yeye ndiye Mungu wao ambaye ana uwezo wa kuwatenganisha na kifo.


