JESHI BURKINA FASO LAMTEUA MWANDISHI WA HABARI NA MTANGAZAJI KUWA WAZIRI MKUU.

Kikosi tawala cha kijeshi cha Burkina Faso hivi karibuni kimemteua Waziri Mkuu mpya wa Nchi hiyo ikiwa ni siku moja baada ya kuvunja serikali bila kutoa sababu yoyote. 

Rimtalba Jean Emmanuel Ouedraogo ambaye alikua Mwandishi wa Habari na baadae waziri wa mawasiliano na msemaji wa serikali, atakuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi, taarifa iliyotolewa na kiongozi wa junta na Rais wa Burkina Faso, Ibrahim Traore iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa Jumamosi.

Traore alitoa amri Ijumaa ya kumfukuza kazi aliyekua Waziri Mkuu Apollinaire Joachim Kyelem de Tambela na kutangaza kufutwa kwa serikali ya kitaifa ambapo mpaka sasa hakuna sababu iliyotolewa kwa hatua hiyo.

Wanajeshi nchini Burkina Faso walichukua mamlaka mnamo Septemba 2022 kwa kuuondoa utawala wa kijeshi wa Luteni Kanali Paul Henri Sandaogo Damiba ikiwa takriban miezi minane baada ya kufanya mapinduzi ya kumuondoa Rais aliyechaguliwa kidemokrasia Roch Marc Kaboré.

Nchi hiyo ni mojawapo ya mataifa kadhaa ya Afrika Magharibi ambapo jeshi limechukua hatamu hivi karibuni, likisema hali hiyo imekuja ikiwa ni kutoridhishwa na serikali za awali zilizochaguliwa kidemokrasia kuhusu masuala ya usalama.

Hata hivyo tangu kuanzishwa kwake, junta imejitahidi kumaliza changamoto za usalama za Burkina Faso sababu ambayo inatajwa kuwa ilichangia kuchukua mamlaka ya nchi hiyo.

Serikali ya mpito ya nchi imekuwa ikiendeshwa chini ya katiba iliyoidhinishwa na bunge la kitaifa lililojumuisha maafisa wa jeshi, mashirika ya kiraia na viongozi wa kimila na kidini.

Chini ya shinikizo kutoka kwa muungano wa kanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS, junta ilikuwa imeweka lengo la kufanya uchaguzi mnamo Julai 2024 ili kurejesha nchi kwenye utawala wa kidemokrasia. Hata hivyo, mwezi Mei iliongeza muda wake wa mpito kwa miaka mitano zaidi, muda wa muhula mmoja wa urais.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *