JENGENI OFISI YA TUME YA UMWAGILIAJI – RAIS SAMIA

Na Saada Almasi -Simiyu 

Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo kwa waziri wa kilimo Hussein Bashe kuhakikisha kunajengwa ofisi ya tume ya umwagiliaji katika mkoa wa Simiyu ili kuharakisha mradi huo ambao unakwenda sambamba na mradi wa kusambaza maji ya ziwa Victoria 

“Huu mradi mkubwa wa umwagiliaji ambao umesema unapita hadi Dodoma nataka ofisi za tume hiyo zijengwe katika mkoa ambao mradi huo napita na kwa kuwa unakwenda sambamba na ule wa maji ya ziwa Victoria naomba ofisi hizo zijengwe mkoani Simiyu ili kuharakisha kukamilika kwake na wananchi wapate huduma”amesema Rais Samia

Amesema kuwa kwa sasa tatizo la maji Simiyu linakwenda kuisha na kubaki historia kwani nguvu kubwa imetumika katika utekelezaji ili mwananchi wa Smiyu apete maji 

“Tumejipanga vyema kuleta maendeleo kwa wananchi na ninakwenda kuweka jiwe la msingi kwenye ule mradi mkubwa wa maji wilayani Busega niwahakikishie tatizo la maji mkoani Simiyu linakwenda kuwa historia kwa sababu kama serikali tumedhamiria kulisimamia hadi kukamilika kwake” ameongeza Rais Samia

Sambamba na hilo Rais Samia ameziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaweka utaratibu mzuri wa vikundi vinavyopaswa kupewa mkopo wa asilimia kumi vipate mkopo huo na si kupata usumbufu unaokwenda kuwakatisha tamaa kwa kuwa na mlolongo mrefu wa kujaza fomu zisizo na faida

“Mtakumbuka miaka miliwi iliyopita nilisitisha utoaji wa mikopo kwa sababu ya kubaini mliwapa mikopo wasiokuwa na sifa mwishowe urejeshaji ukawa mbovu,sasa nawaagiza msiweke mlolongo mrefu wa kujaza fomu na ikiwezekana muwasaidie ili wapate haki ya kuchukua fedha hizi “amesema Rais Samia

Rais Dkt Samia anatarajiwa kuhitimisha ziara yake ya siku tano mkoani Simiyu katika wilaya ya Busega kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa maji wa ziwa Victoria yatakayosambazwa katika maeneo yote ya mkoa huo unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 400.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *