KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake imepitia mwenendo na matukio mbalimbali na kufanya maamuzi yafuatayo
Meneja wa Klabu ya KenGold, Nuhu Nkaekwa amefungiwa michezo mitatu na kutozwa fani ya shilingi laki tano kwa kosa la kumshambulia kwa maneno makali mwamuzi msaidizi namba moja katika mchezo wa KenGold na Pamba kulingana na kanuni ya 45:4(2.11) ya Ligi Kuu pia meneja huyo amefungiwa michezo miwili na kutozwa faini ya shilingi milioni moja kwa kosa la kutoboa mpira mmoja uliokuwa ukitumika katika mchezo huo na atapaswa kulipa mpira mpya kwa mujibu wa kanuni ya 45:2(2.5)ya Ligi Kuu.
Klabu ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera imepewa onyo kali kwa kosa la kuchelewa kuwasili kwenye kikao cha kitaalamu cha maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Namungo disemba 10 mjini Bukoba ambapo Kagera waliwasili saa nne na dakika 10 badala ya saa nne kamili huku adhabu hii ikiwa kwa mujibu wa kanuni ya 1:2(2.2) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za michezo.
Kocha msaidizi wa Azam Bard Eddine ametozwa faini ya shilingi milioni moja kwa kosa la kuvunja paa la benchi la ufundi kwa hasira baada ya mchezo kumalizika katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora wakati wa mchezo wa Tabora United dhidi ya Azam aidha kocha huyo atalazimika kulipa gharama za matengenezo ya paa hilo kwa mujibu wa kanuni ya 45:2(2.5) kuhusu udhibiti wa Makocha.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya JKT Tanzania Jemedari Said amepewa onyo kali kwa kosa la kuingia katika eneo la kimashindano la uwanja wa KMC Complex wakati wa mchezo wa Simba dhidi ya JKT ukiendelea.
Kiongozi huyo alishuka kutoka jukwaani na kwenda hadi eneo la benchi la ufundi la klabu yake kwa lengo la kuzungumza na viongozi kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:17 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za michezo
Klabu ya JKT Tanzania imetozwa faini ya shilingi milioni 5 kwa kosa la wachezaji wake kuonywa kwa kadi zaidi ya mara tano katika mchezo wa Simba dhidi yaoambapo JKT walionywa kwa kadi mara saba na adhabu hii ikiwa ni kwa mujibu wa kanuni ya 47:10 ya Ligi Kuu.
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu imempa onyo kali Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga Abdihimid Moallin kwa kosa la kuketi kwenye benchi la ufundi katika michezo mitatu ya Ligi Kuu ya NBC kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:17 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za michezo adhabu imetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 17:62 kuhusu taratibu za michezo.
Aidha Bodi ya Ligi Kuu imepokea taarifa kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa klabu ya Yanga imekamilisha taratibu zote za kumtumia Abdihamid Moallin kama kocha msaidizi.
Kwa upande wa Ligi ya Championship Mchezaji Pascal Mwakapusya wa klabu ya Mbuni, amefungiwa michezo mitano na kutozwa faini ya Shilingi milioni moja kwa kosa la kumpiga mwamuzi msaidizi namba mbili, Leah Petro wa mchezo kati ya Mbuni FC na Mtibwa Sugar FC kabla hajaokolewa na walinzi wa uwanjani (stewards) 1adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 41:5(5.3) ya Ligi ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Klabu ya Mbuni ya mkoani Arusha imetozwa faini ya shilingi milioni moja kwa kosa la mashabiki wake kumshambulia kwa matusi na kumpiga mwamuzi msaidizi namba mbili (2), Leah Petro wa mchezo tajwa hapo juu, kabla hajaokolewa na walinzi wa uwanjani (stewards) adhabu hii ni kwa kuzingatia Kanuni ya 47:1 ya Ligi ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Klabu ya Biashara United ya mkoani Mara imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Shilingi milioni tatu na kupoteza mchezo wa Mbeya City FC dhidi ya Biashara United FC na kupokwa alama 15 (kumi na tano) katika msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC 2024/2025, kwa kosa la kushindwa kufika kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya bila sababu za msingi, jambo lililosababisha mchezo huo usifanyike.
Biashara iliiandikia barua Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kuomba mchezo huo ambao awali ulipangwa kufanyika Desemba 1, 2024 usogezwe mbele na ombi lao likakubaliwa ambapo mchezo huo ulipangwa kufanyika Desemba 3, 2024 hata hivyo klabu ya Biashara United haikufika uwanjani katika tarehe hiyo mpya, hivyo maofisa wa mchezo huo kuahirisha mchezo kwa mujibu wa Kanuni.
Kufuatia maamuzi hayo ya kamati, klabu ya Mbeya City imepewa alama tatu na mabao matatu adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 31:1 ya Ligi ya Championship kuhusu Kutofika Uwanjani.
Kocha wa magolikipa wa klabu ya Geita Gold, Augustino Malindi amefungiwa michezo 16 (kumi na sita) na kutozwa faini ya Shilingi milioni moja kwa kosa la kumshika sehemu za siri mwamuzi wa akiba wa mchezo wa Mbeya City FC 1-0 Geita Gold FC, baada ya kuonywa kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumtukana mwamuzi msaidizi namba moja wa mchezo huo.
Kocha huyo alitenda kosa lingine akiwa anakwenda vyumbani baada ya kuonywa kwa kadi, kwa kumshika kifuani mratibu wa mchezo huo (GC) ambaye ni mwanamke jambo ambalo ni kinyume na maadili ya ukocha na mpira wa miguu kwa ujumla adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 45:2(2.1) ya Ligi ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
Pia kocha Augustino Malindi amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Shilingi laki tano kwa kosa la kumtukana mwamuzi msaidizi namba moja wa mchezo huo jambo lililosababisha aonywe kwa kadi nyekundu adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 45:2(2.11) ya Ligi ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
Kwa upande wa First League Kocha wa klabu ya African Lyon, Elia James amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Shilingi laki tano kwa kosa la kuwatukana waamuzi wa mchezo wa Hausang FC 1-0 African Lyon FC jambo lililosababisha aonywe kwa kadi nyekundu adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 45:2(2.11) ya First League kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
Golikipa wa akiba wa African Lyon, Ibrahim Bigambo amefungiwa michezo mitano na kutozwa faini ya Shilingi laki tano kwa kosa la kumpiga ngumi mchezaji wa klabu ya Hausang, kisha kwenda kujificha ndani ya chumba cha kuvalia cha klabu yake adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 46:3 ya Ligi ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Viongozi.