Na Faustine Kasala – Kigoma.
Jamii imetakiwa kutovifumbia Macho vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Wasichana, ili makundi hayo yaweze kufikia malengo yake kiuchumi na Kielimu sambamba na kuleta mabadiliko chanya katika vitendo hivyo
Akizungumuza na Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Kigoma katika Mafunzo juu ya mchango wa vyombo vya habari katika kutatua changamoto za Ukatili dhidi ya Wanawake na wasichana, Meneja wa Mradi wa Wezesha Biti kutoka Shirika la Kivulini, Grace Musa amesema Moja ya Changamoto zinazo changia kuendelea kuwepo kwa vitendo vya Ukatili ni pamoja na ukubalikaji wa vitendo hivyo katika Jamii.
‘Amesema, ‘kwa ujumla vyanzo vya ukatili vinaweza kuwa ni vingi lakini sisi kama Shirika la Kivulini tumegundua kuwepo wa vitendo vya ukatili ambavyo vinaonekana kukubalika katika jamii, na jamii haioni kama ni ukatili katika makundi haya, mfano ukatili wa Kisaikolojia, ukatili wa kingono ukatili wa kimwili na mengine mengi ambayo hayatolewi taarifa katika mamlaka husika, hivyo tunajitahidi sasa kuhakikisha kuwa jamii mambo kama haya inayatambua.”

Aidha, Grace amesema katika utekelezaji wa Mradi huo wamekuja na mbinu mpya iitwayo SASA ambayo inatambua mchango wa kumshirikisha kila mtu bila kujali rika, umri, jinsi, kabila, rangi dini na hata uwezo wa kifedha kuanzia mtu mmoja mmoja vikundi na hata mashirika.
Amesema mbinu ya SASA itawasaidia pia wana jamii kuweza kutoa msaada kwa wahanga wa matukio ya ukatili ikiwa ni pamoja na kuwaelekeza wapi pa kwenda kupata msaada wa kisheria na hata wakati mwingine kujitoa muhanga kwa wahanga hao kuwapeleka katika huduma za kwanza za matukio ya Ukatili.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Kigoma, Jackob Luvilo amesema Wanaume wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ukatili kwani wao ndio wamekuwa watuhumiwa wa kwanza katika utekelezaji wa vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.

”Kwa mtazamo wangu wanaume wanapaswa kuongoza Jahazi la Mapambano dhidi ya ukatili na suala hili ni la kielimu zaidi kwani mapokeo ya mila na Tamaduni kuwa mwanaume ni kichwa cha familia imekuwa ni chanzo cha ukatili katika baadhi ya ndoa na mahusiano, japo sina maana kuwa kila ukatili unaotendeka sababu ni hiyo hapana, ila kwa kiwango kikubwa tuanze na wanaume kuwaelimisha,'” alisema.
Mradi wa wezesha binti unatekelezwa na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Kivulini katika Halmashauri tatu za Mkoa wa Kigoma ikiwemo Halmashauri ya Mji Kasulu, Halmashauri ya Kibondo na Halmashauri ya wilaya ya Kasulu kwa kushirikiana naTaasisi ya ushirikiano wa Kimataifa ya Enabel ukilenga mamlaka za serikali, viongozi wa kijamii, Jamii na Familia kukuza utamaduni wa kuzuia ukatili na unyanyasaji kwa wanawake na wasichana


