JAMII YATAKIWA KUACHANA NA VITENDO VYA UKATILI MAJUMBANI

Na Adam Msafiri, Musoma – Mara.

Katika jitihada za kukabiliana na ongezeko la matatizo ya afya ya akili kwa watoto na vijana, wazazi mkoani Mara wametakiwa kuachana na vitendo vya ukatili majumbani, ikiwemo vipigo, matusi na mateso ya kisaikolojia.

Mratibu wa mradi wa Ni Sawa Kutokuwa Sawa, Dorothy Deus amesema vitendo hivyo vinaathiri kwa kiasi kikubwa afya ya akili ya watoto na vijana na mara nyingi huwafanya kukimbilia mtaani au kuishi katika msongo wa mawazo unaoweza kusababisha ugonjwa wa akili.

Mratibu wa mradi wa Ni Sawa Kutokuwa Sawa, Dorothy Deus.

“Vipigo,mateso na manyanyaso makali kwa watoto na vijana majumbani mwao hupelekea wengi wao kuwa na stress,kuishi mitaani na wakati mwingine kupata matatizo ya afya ya akili. Ninashauri wazazi na walezi wajitahidi kuepuka migogoro ya kifamilia na kuacha kabisa ukatili dhidi ya watoto,” amesema Dorothy.

Ameongeza kuwa,mradi huo unaendelea kutoa elimu katika shule mbalimbali za sekondari mjini Musoma ili kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu namna ya kutambua na kukabiliana na changamoto za afya ya akili.

Kwa upande wake,Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Musoma, Fred Isaya,amekiri kushuhudia ongezeko la watoto wanaoamua kuondoka majumbani na kuishi mitaani kutokana na ukosefu wa malezi bora na ukatili wa kifamilia.

“Tumeona idadi ikiongezeka ya watoto wanaoishi mitaani kutokana na kukosa upendo na malezi mazuri. Familia zinapaswa kutimiza wajibu wao katika kulea, kulinda na kuwalinda watoto dhidi ya ukatili,” amesema Isaya.

Wakati huo huo,wanafunzi wa Shule ya Wasichana ya Songe wameeleza kufurahishwa na elimu hiyo,wakisema imewasaidia kuelewa jinsi ya kutambua dalili za msongo wa mawazo na namna ya kujitunza kisaikolojia.

Mradi wa Ni Sawa Kutokuwa Sawa unaendelea kufanyika katika shule mbalimbali za sekondari mjini Musoma,ukiwa na lengo la kupunguza unyanyapaa na kuongeza uelewa kuhusu afya ya akili miongoni mwa vijana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *