Jamii imetakiwa kuendelea kufichua vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto hatua itakayowezesha hatua sahihi kuchukuliwa ili kutatua changamoto hiyo ndani ya Jamii.
Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Shinyanga Ngasa Mboje ametoa rai hiyo April 17,2024 wakati akizungumza katika kikao cha wadau wa ukatili pamoja na kupokea na kujifunza juu ya utafiti wa Citizen for Change na Women Fund Tanzania, kikao kilichoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa habari Shinyanga kwa ufadhili wa Women Fund Trust.
Mratibu wa Mfuko wa Ruzuku wa Wanawake Tanzania (WFT-Trust) mkoani Shinyanga Glory Mbia, amesema tangu mwaka 2019 wamekuwa wakitoa Ruzuku kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya kutokomeza ukatili wa kijinsia ndani ya jamii na kuonyesha kuridhishwa na matokeo ya kupinga kwa ukatili.
Nae Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Edmund Ardon, akimwakilisha Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii wilayani humo
amesema Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga inawapongeza wadau mbalimbali wa Maendeleo wakiwemo waandishi wa habari kwa kuendelea kutekeleza Miradi ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa Kijinsia ndani ya jamii kwa kusaidiana na Serikali katika utekelezaji wa mpango wa (MTAKUWWA) na kuleta ukombozi kwa wanawake na watoto.
Awali kupitia hotuba ya ufunguzi wa kikao hicho Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga Greyson Kakuru, ameupongeza Mfuko wa Ruzuku wa Wanawake Tanzania (WFT-Trust), kwa kuendelea kushirikiana nao na kuwapatia Ruzuku ya kutekeleza miradi ya kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Amesema ndani ya miaka mitatu mfululizo ya utekelezaji wa Miradi hiyo, wameweza kuandika habari 355 ambazo zimeleta mabadiliko chanya ndani ya jamii na kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia wilayani Shinyanga.