Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Kampuni ya Jambo Group ya mjini Shinyanga imeingia mkataba wa kuidhamini timu ya Dodoma jiji kwa kipindi cha mwaka mmoja katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (NBC Premier League), 2026/2027, uliosainiwa leo mjini Shinyanga.
Akizungumza wakati wa utiaji saini Mkataba huo, Mkuu wa Ubunifu wa Mikakati na Chapa ambaye pia ni Meneja Mkuu wa Jambo Media, Nickson George amesema, wameamua kurefusha ushirikiano wao na Dodoma Jiji, baada ya kuridhishwa na mwenendo wa timu hiyo.

“Tumeingia mkataba huu kwa mara nyingine tena na Dodoma Jiji, ili kuendelea kuwaunga mkono katika msimu mpya wa ligi kuu. lengo letu ni kuona klabu hii inafikia malengo yake,” amesema George.
Naye Mtendaji Mkuu wa Dodoma Jiji, Albert Kasoga ameishukuru Jambo Group kwa kuendelea kuwaamini na kuwekeza kwenye sekta ya michezo nchini, huku akiahidi kuwa timu hiyo itafanya vizuri zaidi msimu ujao wa ligi kuu.

Amesema, “tunamshukuru sana mdhamini wetu Jambo Group kwa kuendelea kuwa nasi. Tunaahidi kupambana na kufanya vizuri zaidi katika msimu huu mpya.”
Kwa upande wake, Afisa Habari na Msemaji wa Dodoma Jiji, Moses Mpunga amesema, udhamini huo umekuwa nguzo muhimu katika uendeshaji wa timu na utasaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha shughuli za klabu hiyo.

“Msimu uliopita ulikuwa msimu mzuri kwetu tukiwa chini ya udhamini wa Jambo Group. Kupitia ushirikiano huo, timu iliweza kufanya vizuri katika vipindi tofauti, na yote haya ni matokeo ya ushirikiano wetu. Kwa hiyo, kuongezwa kwa mkataba huu wa awamu ya pili kutatusaidia kufanya vizuri zaidi katika msimu unaofuata,” amesema Mpunga.
Ameongeza kuwa, mbali na kusaidia shughuli za michezo, Jambo Group imeendelea kuisapoti Dodoma Jiji katika maeneo mengine ya kijamii ikiwemo afya na usafi wa mazingira.

“Kupitia ushirikiano huu, Jambo Group imeweza kutusapoti pia katika sekta nyingine kama afya pamoja na usafi wa mazingira, kwa kutupatia vifaa na T-shirt. Kwa hiyo, kupitia ushirikiano wetu huu, tunaamini tunaweza kufanya vizuri zaidi,” alisema Mpunga.
Amesema klabu hiyo inajiandaa kuandaa mechi maalumu kubwa itakayofanyika mkoani Shinyanga chini ya udhamini wa Jambo Group, ikiwa ni sehemu ya kuwapongeza na kuwazawadia mashabiki wa soka wa mkoa huo.

Kuongezwa kwa mkataba huo kunadhihirisha dhamira ya Jambo Group ya kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya michezo nchini, huku Dodoma Jiji ikitarajia kutumia ushirikiano huo kama chachu ya kufanya vizuri zaidi katika msimu wa ligi 2026/2027.


