JAMBO GROUP YAENDELEZA UDHAMINI LIGI KUU, NI ZAMU YA DODOMA JIJI

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Kampuni ya Jambo Food Products imeendelea kuonesha mchango wake, katika kukuza michezo nchini, baada ya kutangaza rasmi kuidhamini Klabu ya Soka ya Dodoma Jiji, inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2025/2026.

Mkataba huo wa mwaka mmoja, umesainiwa hii leo Septemba 23, 2025 kati ya Viongozi wa Jambo Food Products na Dodoma Jiji FC, katika ofisi za Kampuni zilizopo Kata ya Ibadakuli, Manispaa ya Shinyanga.

Akizungumza wakati wa utiaji saini, Msimamizi wa Chapa na Ubunifu wa Jambo Group, Nickson George amesema kampuni hiyo imeendelea kuzisaidia timu mbalimbali nchini na sasa imeamua kuishika mkono Dodoma Jiji FC, ili kufanikisha ndoto na malengo yao kwenye Ligi Kuu.

Hatua hii siyo tu udhamini, bali ni ushirikiano wa kibiashara na kijamii utakaosaidia kukuza chapa za pande zote mbili kupitia michezo. Dodoma Jiji FC sasa ni sehemu ya familia ya Jambo Group – ‘Jamukaya’, na Jambo Group ni sehemu ya Dodoma Jiji FC,” amesema Nickson.

Kwa upande wake Kiongozi wa Dodoma Jiji FC, Dickson Kimaro ameishukuru Jambo Group kwa kuiamini timu yao na kuahidi kuitangaza vyema chapa ya kampuni hiyo kupitia matokeo mazuri katika msimu huu wa ligi.

Kampuni ya Jambo  group imekuwa ni mdau mkubwa wa soka nchini na imekuwa ikidhamini timu mbalimbali za ukanda wa ziwa ambapo hivi karibuni imeingia makubaliano ya kuwa mdhamini mkuu wa timu ya Pamba jiji FC ya jiji ya jijini Mwanza kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *