Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Mgombea Ubunge Jimbo la Meatu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Salum Khamis maarufu Jambo, amemuombea kura nyingi za ushindi Mgombea Urais wa CCM Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,Mgombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi na Mgombea Udiwani Kata ya Mjini, Jimbo la Shinyanga Mjini Salum Kitumbo.
Jambo ameomba kura hizo leo Oktoba 17,2025, kwenye Mkutano wa Kampeni wa Mgombea Udiwani wa Kata ya Mjini, Jimbo la Shinyanga Mjini Salum Kitumbo, uliofanyika viwanja vya Soko Kuu la Mjini Shinyanga na kuhudhuriwa na Mamia ya wananchi.

Amewaomba wananchi kwamba,siku ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 wajitokeze kwa wingi kupiga kura kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Patrobas Katambi pamoja na Salum Kitumbo, ili wapate kuwaletea maendeleo kwa sababu ni viongozi makini na wenye kujali maslahi ya watu.
“Ndugu zangu wananchi wa Shinyanga Mjini, Oktoba 29 nendeni mkapige kura kwa sababu ni haki yenu ya msingi na mkawachague wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya Rais,Wabunge na Madiwani,” amesema Khamis.

Akimzungumzia Rais Samia, amesema ndani ya utawala wake wa miaka mitano amefanya mambo makubwa, pamoja na kuiletea maendeleo Kata ya Mjini, huku akimpongeza pia Patrobas Katambi kwa uongozi mzuri.
Kwa upande wa Salum Kitumbo, amesema anamfahamu vizuri na kwamba Kata ya Shinyanga Mjini imepata Diwani ambaye ni mchapakazi, Mwaminifu, Mwadilifu na ambaye anajali maslahi ya watu sababu amefanya naye kazi siku nyingi na anamfahamu vizuri.

“Salum Kitumbo nasimama hapa kukuombea kura kwa wananchi wa kata ya Mjini,nina imani watakupatia ridhaa ya kuwa diwani wao,na kazi ya udiwani ni utumishi wa watu, nakuomba sana ukawatumikie wananchi,simu zipatikane na nyumbani kwako upatikane. kashughulikie matatizo ya wananchi na uwaletee maendeleo nafahamu utendaji wako kazi, sina mashaka na wewe,” amesema Salum.
Naye Mgombea Udiwani Kata ya Mjini, Salum Kitumbo ameahidi kwamba atakamilisha ujenzi wa Soko Kuu la Mjini humo, ili kuboresha mazingira rafiki kwa Wafanyabishara.

Ametoa ahadi nyingine kwamba barabara zote za mjini humo zitajengwa kwa kiwango cha lami katika mitaa yote, huku akiwaahidi pia kusimamia suala la mikopo ya Halmashauri ya asilimia 10, ili makundi husika ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu wapate kunufaika na kuinuka kiuchumi.


