JAMBO ATAKA KASI MRADI WA UJENZI SHULE YA SEKONDARI MALUGALA

Na Saada Almasi, Meatu – Simiyu.

Mbunge wa Jimbo la Meatu, Salum Khamis Jambo ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondani katika kitongoji cha Malugala Kata ya Mwanhuzi Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, ambao unatekelezwa na serikali kwa lengo la kujiandaa kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka wa masomo 2028.

Akiwa katika eneo la mradi huo unaogharimu zaidi shilingi milioni 500, Jambo amemtaka Mkandarasi Think Time kutekeleza ndani ya wakati, kwani uhitaji wa madarasa hayo ni mkubwa kutokana na mabadiliko ya mitaala ya kimasomo, inayoruhusu wanafunzi kujiunga kidato cha kwanza baada ya kumaliza darasa la sita.

“Mnajua kutakuwa na madarasa mawili kujiunga na elimu ya sekondari 2028 na kutokana na hilo maandalizi kama haya ni muhimu sana na hizi pesa ambazo zimetolewa zimeelekezwa katika maeneo mengine pia kwa mradi kama huu kwa hiyo nikuombe muda ambao umeainishwa na mkataba wa miezi mitatu kazi hii ikamilike,” amesema Salum Jambo.

Ameongeza kuwa, “kunapokuja na pesa nyingi ya serikali mahali fulani tambueni kuwa kuna macho mengi ambayo yanawatizama na kila mgeni ama kiongozi ambaye atafika Meatu ataelekezwa kufika kuona maendeleo ya mradi kwa hiyo ondoeni vikwazo ambayo mnaweza kuviepuka mradi uishe kwa pesa ambazo mmeafikiana kama kuna changamoto ambazo nitapaswa kuondoka nazo niwaahidi nitazibeba na kuzifikisha mahali husika ili zishughulikiwe ipasavyo.”

Kwa mujibu wa taarifa ya mkandarasi wa mradi huo zipo changamoto ambazo zinaukumba mradi ikiwa ni pamoja na mlipuko wa bei ambao unapelekea kupanda kwa baadhi ya vifaa vya ujenzi kama sementi na madini ujenzi kama mchanga na kokoto sambamba na uhaba ya maji katika eneo hilo hali ambayo inawalazimu kununua maji badala ya kutumia maji ya mamlaka.

Mradi wa Shule ya Sekondari kitongoji cha Malugala, umeanza Julai 2026 baada ya maelekezo kutoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kwa ufadhili wa programu ya Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari  (SEQUIP) na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu ili kujiandaa kupokea wanafunzi wanaotarajiwa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2027.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *