Wakili wa Taifa la Israel katika kesi iliyofunguliwa na Afrika Kusini katika Mahakama ya ICJ Bw.Gilad Noam.
Israel imejitetea mbele ya mahakama ya ICJ kuhusu hatua ya vikosi vyake vya jeshi kuendelea na operesheni yake Gaza baada ya Afrika Kusini kuwasilisha kesi ikiitaka Israel kusitisha kabisa oparesheni yake ya kijeshi.
Januari mwaka huu mahakama hiyo iliiagiza Israel kuhakikisha kwamba wanajeshi wake hawafanyi mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina wakati wa operesheni yake ya kijeshi na pia ilitakiwa iruhusu misaada zaidi kuingia ndani ya Ukanda wa Gaza.
Afrika Kusini imeihimiza mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa itoe amri ya kusitishwa kwa operesheni hiyo ya mjini Rafah na kuitaka Israel iondoe wanajeshi wake mara moja wakati Israel imesisitiza kuwa oparesheni hiyo ni muhimu katika azma yao ya kulitokomeza kabisa kundi la Hamas.
Mkurugenzi wa idara ya uhusiano wa Afrika Kusini Zane Dangor, Waziri wa mambo ya nje wa Afrika Kusini Naledi Pandor na balozi wa Afrika Kusini nchini Uholanzi Vusimuzi Madonsela wakifuatilia Shauri ambalo Taifa lao limefungua dhidi ya Israel.
Leo Ijumaa Mei 17,2024, Israel imejibu tuhuma zinazoikabili serikali ya mjini Jerusalem ikiwemo mauaji ya halaiki, mateso na kuzuia kwa makusudi misaada ya kibinadamu kupelekwa ukanda wa Gaza na kueleza kwamba kesi hiyo dhidi yake haijazingatia ukweli wa mambo na wakili wa Israel Gilad Noam ameitaja kesi hiyo kama dhihaka kwa mkataba wa mauji ya Kimbari wa Umoja wa Mataifa.
Hii ni kesi ya tatu inayohusu vita kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas tangu Afrika Kusini ilipowasilisha kesi ya jinai dhidi ya Israel kwa mara ya kwanza mwezi Disemba mwaka jana
Mahakama hiyo ya kimataifa ya haki (ICJ) inaendelea kutathmini iwapo vitendo vya Israel katika ukanda wa Gaza vinakiuka mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1948 kuhusu mauaji ya kimbari.