Israel na Iran wazua hofu ya vita ya tatu ya dunia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana kwa dharura Jumapili Aprili 14, saa kumi jioni kwa saa za New York Marekani kwa lengo la kujadili hali ya Mashariki ya Kati kufuatia shambulio la Iran dhidi ya Israel.


Kupitia Mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amehutubia wajumbe wa Baraza hilo na kusisitiza kwamba si ukanda (Mashariki ya kati) wala ulimwengu una0weza kumudu vita zaidi.


Amesisitiza kwamba mashariki ya kati ipo kwenye ukingo wa kuporomoka, watu katika eneo hilo wanakabiliwa na hatari halisi ya mzozo mkubwa na sasa ni wakati wa kutuliza hali hiyo, Sasa ni wakati wa kujizuia zaidi ilhali balozi wa Israel ameutumia muda wake kulilaumu Baraza la Usalama kwamba alitahadharisha mapema na mara nyingi kuhusu Iran lakini hawakumsikiliza.


Nae mwakilishi wa Iran ameeleza kwamba hatua waliyoichukua ya kurusha makombora dhidi ya Israel yalikuwa kitendo cha kujilinda ambacho kinakubalika kimataifa na kuzitupia lawama nchi za Marekani,Ufaransa na Uingereza akidai zimechagua kwa mara nyingine tena kuufumbia macho ukweli na kutoangalia sababu kuu zinazochangia hali ya sasa.


Jumamosi usiku Aprili 13, Iran ilirusha zaidi ya ndege mia tatu zisizo na rubani(drones), makombora dhidi ya Israel kujibu shambulio kubwa la anga ambalo Iran iliihusisha Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus, Syria, wiki mbili zilizopita.

Mataifa mbalimbali duniani yamekuwa na maoni na mitazamo tofauti tofauti juu ya kinachoendelea Ukanda wa Gaza, Colombia inaona kama ni kiashiria cha Vita Kuu ya Tatu ya Dunia, huku Urusi, China, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Papa Francis wakisisitiza utulivu.


Msimamo wa Marekani, Uingereza, Ujerumani, Canada na Argentina umekuwa ni kuiunga mkono Israel katika kipindi hiki ambacho utawala wa Iran kupitia wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imewaita na kuwahoji mabalozi wa Uingereza,Ufaransa na Ujerumani waliopo Tehran ikiwatuhumu kwa kutowajibika juu ya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel.

Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kupitia Mwanadiplomasia wake Mkuu Josep Borrel kupitia akitumia ukurasa wake wa Mtandao wa X amesema hilo ni ongezeko lisilo kifani la tishio la kikanda aisdha Urusi iliyo katika mapigano na Ukraine pia imetoa maoni yake juu ya kinachoendelea kati ya Iran na Israel ikisema kwamba inasikitishwa na mashambulizi ya Iran na kutaka pande zote kujizuia.


Kiini cha yanayoendelea kati ya Iran na Israel ni Aprili Mosi ya Mwaka huu baada ya kutokea kwa mashambulizi ya anga katika ubalozi wa Iran uliopo Damascus nchini Syria na kusababish vifo vya watu 13 wakiwamo majenerali wawili wa Jeshi la Iran ambapobaada ya tukio hilo Iran ilisisitiza kwamba mhusika(ambaye ni Israel) atawajibishwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *