Israel imefanya mashambulizi ya usiku kucha katika Ukanda wa Gaza, huku jeshi lake likisema halitopoteza mwelekeo katika vita vyake Gaza kutokana na shambulio la Iran ambalo halijawahi kushuhudiwa.
Wakati wapatanishi wakiendelea kutafuta suluhu ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza yaliochochewa na shambulio la Hamas la Oktoba 7, hofu imeongezeka kwa Israel kupeleka wanajeshi zaidi katika mji wa kusini mwa Gaza Rafah ambako wakazi zaidi ya milioni 2.4 wa eneo hilo wamekimbilia ili kujilinda na mapigano yanayoendelea.
Msemaji wa Jeshi la Israel Daniel Hagar amesema kwamba licha ya mashambulio ya Iran, hawajapoteza lengo lao katika vita vyake ndani ya Ukanda wa Gaza katika kuwaokoa mateka takriban 130, ikiwemo 34 wanaohofiwa kuuwawa, ambao Israel inasema wamesalia katika mikono ya kundi la Hamas.
Hagari ameongeza kwamba jeshi litaongeza vikosi zaidi vya akiba kwa ajili ya ufanisi wa shughuli zake za kijeshi katika eneo la Rafah, ikiwa ni wiki moja tu tangu kuondoa idadi kubwa ya wanajeshi wakwe wa ardhini katika eneo hilo.
Hadi sasa hakuna makubaliano yoyote yalioafikiwa kati ya Israel na Hamas huku msimamo wa pande zote mbili ikiwa haujabadilika.
Awali Hamas ilikataa mapendekezo yote ya maafikiano yaliotolewa na Israel ikisisitiza kukomeshwa kabisa kwa mapigano na Israel kuondoa kikamilifu wanajeshi wake katika eneo la Ukanda wa Gaza.