Iran imeikumbusha Israel imeiarifu Israel kwamba endapo itachukua hatua ya kuishambulia tena Tehran itakuwa tayari kujibu mapigo ndani ya muda wa sekunde chache katika wakati huu ambao Jumuiya ya kimataifa imeendelea kutoa kauli za kuiunga mkono Israel.
Ndani ya Israel ripoti zinasema baraza la mawaziri lenye jukumu la kusimamia vita linajiandaa kukutana kwa mara ya tatu leo katika kipindi cha siku tatu katika kikao ambacho kinalenga kutoa maamuzi kuhusu hatua zitakazochukuliwa dhidi ya Iran,kikao ambacho kinafanyika wakati jumuiya ya kimataifa inaishinikiza Israel kujiepusha kuutanuwa mgogoro katika kanda nzima ya Mashariki ya Kati.
Tanngu Jumamosi,Mkuu wa majeshi wa Israel Herzi Halevi alitoa ahadi kwamba nchi hiyo itachukuwa hatua kujibu mashambulizi ya zaidi ya makombora 300, droni na maroketi yaliyofyatuliwa na Iran dhidi ya nchi hiyo, japo hakutoa ufafanuzi wa kitakachofanyika.
Hii leo Jumanne Marekani na washirika wake wa Umoja wa Ulaya kwa pamoja wameshikamana katika hatua ya kutangaza vikwazo vikali zaidi vya kiuchumi na kisiasa dhidi ya Iran, kama hatua ya kuishawishi Israel kujiepusha na ulipizaji kisasi.
Wakati huo huo,Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameutolea mwito Umoja wa kupitisha vikwazo vipya dhidi ya mifumo ya teknolojia ya uundaji droni ya Iran akikumbusha kwamba umoja huo ulikubaliana mwaka jana kupitisha vikwazo hivyo na kwa hivyo sasa ndio wakati sahihi.