Na Saulo Stephen – Singida.
Wananchi wa Iramba mkoani Singida wameipongeza Serikali kwa kutoa zaidi ya shilingi Bilioni sita kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa daraja la Nkonkilangi, mradi unaolenga kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji ili kukuza uchumi vijijini na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii.
Wakizungumza na Jambo Media wananchi hao wamesema mradi huo umeleta mabadiliko makubwa katika maisha yao ya kila siku.

Aidha wanufaika wa daraja hilo wameeleza kuwa kabla ya ujenzi wake kukamilika walikumbana na changamoto kubwa hasa wakati wa msimu wa masika, ambapo mawasiliano kati ya Wilaya za Iramba, Mkalama na Kishapu yalikatika kabisa, hali iliyodhoofisha biashara, shughuli za kilimo na upatikanaji wa huduma muhimu.
Wamesema iliwalazimu wakati mwingine kukodi watu kubeba wagonjwa kwa mikono ili kuwavusha kwenye mto.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ntwike, Ramadhan Kitulo, pamoja na Halima Maswi, mkazi wa Kijiji cha Nkonkilangi, wameeleza furaha yao kutokana na kukamilika kwa daraja hilo na kubainisha jinsi maisha yalivyokuwa magumu awali kabla ya mradi huo.
Aidha, wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara.



