Mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi, umetangwazwa rasmi na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), na itaanza kupokea mapendekezo kuanzia Februari 27, 2025 hadi Machi 26, 2025.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele ameyasema hayo hii leo Februari 26, 2025 wakati akihitimisha kikao cha Tume, kilichofanyika mkoani Morogoro.
Amesema, “kwa kuzingatia masharti ya Kanuni ya 18(1) ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za mwaka 2024, napenda kutoa taarifa kwa umma kwamba, kuanzia kesho siku ya Alhamisi tarehe 27 Februari, 2025 Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi itaanza mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi.”

Kuhusu muda wa kupokea maombi, Jaji Mwambegele amesema maombi yote ya kugawa au kubadilisha jina la jimbo yawasilishwe Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuanzia tarehe 27 Februari, 2025 hadi tarehe 26 Machi, 2025.
Aidha, amebainisha kuwa Tume inatekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa ibara ya 74(6)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na kifungu cha 10(1)(d) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024, ambapo Tume imepewa jukumu la kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa Wabunge.

Kwa mujibu wa ibara ya 75(4) ya
Katiba, Jaji amesema jukumu hilo la kuchunguza mipaka na kugawa Jamhuri ya Muungano katika majimbo ya uchaguzi linaweza kufanywa na Tume mara kwa mara na angalau kila baada ya miaka kumi.
“Kwa kuzingatia masharti hayo ya Katiba, kwa mara ya mwisho Tume ilichunguza mipaka na kugawa
majimbo ya uchaguzi katika Jamhuri ya Muungano mwaka 2015, ambapo majimbo mapya 26 yalianzishwa,” amesema.

Aidha, Jaji Mwambegele pia amewakumbusha wadau wote
wenye maombi wahakikishe kuwa mapendekezo yanajadiliwa katika Kamati ya Ushauri ya Wilaya, kisha yawasilishwe kwa Katibu Tawala wa Mkoa kwa ajili ya kujadiliwa katika Kamati ya Ushauri ya Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa awasilishe Tume
mapendekezo yaliyopitishwa na kikao cha Kamativya Ushauri ya Mkoa pamoja na viambatisho vyote.
