Na Gideon Gregory – Dodoma.
Tume Huru ya Uchaguzi Nchini, imetangaza kuanzisha Majimbo mapya ya uchaguzi nane katika Mikoa mbalimbali, ambapo kwa Mkoa wa Dar es salaam yameanzishwa Majimbo mawili ya Kivule na Chamazi.
Taarifa hiyo, imetolewa hii leo Mei 12, 2025 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Jacobs Mwambegele.

Amesema, “Mkoa wa Dar es salaam yameanzishwa majimbo mawili, Jimbo la Ukonga limewaganywa na kuanzishwa jimbo jipya la Kivule, pia Jimbo la uchaguzi la Mbagala limewagawanywa na kuanzishwa jimbo jipya la uchaguzi la Chamazi.”
Majimbo mapya yatakuwa sehemu ya Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, ambapo Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani Jacob Mwambegele, amesema tume yake imefikia uamuzi huo baada ya kupitia maombi kutoka kwenye mikoa mbalimbali nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Jaji Mwambegele amesema uamuzi huo umefanyika kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 75(1), (2) na (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Kanuni ya 18(7) ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024.
Ameyataja majimbo hayo kuwa ni Jimbo la Kivule amabalo limegawanywa kutoka Jimbo la Ukonga na Jimbo la Uchaguzi la Chamazi lililogawanywa kutoka Jimbo la Mbagala yote ya mkoani Dar es Salaam.
“Mkoani Dodoma limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Dodoma Mjini limegawanywa na kuanzishwa jimbo jipya la Uchaguzi la Mtumba na Mkoani Mbeya limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Mbeya Mjini limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Uyole,” amesema.
Jaji Mwambegele ameongeza kuwa, Mkoani Simiyu limeanzishwa jimbo jipya moja ambapo Jimbo la Uchaguzi la Bariadi limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la uchaguzi la Bariadi Mjini.
“Huko Geita yameanzishwa majimbo mawili, Jimbo la Busanda limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Katoro na Jimbo la Chato likigawanywa pia na kuanzishwa Jimbo jipya la Chato Kusini.
“Mkoani Shinyanga limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Solwa limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Itwangi,” amesema Jaji Mwambegele mbele ya wanahabari