Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza kumuengua mgombea urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina katika uchaguzi Mkuu wa mwa ka huu 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo Septemba 15, 2025 na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima imeeleza kiwa jina la Mpina limeondolewa kutokana na pingamizi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari.
Katika taarifa hiyo, pingamizi lililowekwa na mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha NRA, Almas Kisabya dhidi ya mgombea wa Kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina limetupiliwa mbali.

Kuhusu pingamizi lililowekwa na Kunje Ngomale Mwiru (mgombea kiti cha Rais kupitia chama cha AAFP), dhidi ya Luhaga Mpina (mgombea wa Kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT Wazalendo), Tume pia imekataa na kutupilia mbali.
Aidha, pingamizi lilowekwa na Luhaga Mpina dhidi ya Dkt. Samia Suluhu Hassan (mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), limekataliwa na kutupilia mbali na tume.
Hata hivyo, Tume imekubali pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari dhidi ya uteuzi wa Luhaga Mpina kuwa mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.