Na Clavery Christian, Bukoba – Kagera.
Menejimenti ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba imezitambua na kuzipongeza idara, vitengo pamoja na watumishi waliofanya vizuri katika kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Hafla hiyo, iliyoandaliwa na Kitengo cha Usimamizi wa Ubora wa Huduma (Quality Improvement Unit – QIU), imelenga kuthamini juhudi za watumishi na vitengo vilivyoonyesha kiwango cha juu cha uwajibikaji, weledi na kujituma katika kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora, salama na zenye kukidhi viwango vinavyotakiwa.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Ubora wa Huduma (QIU), Bi. Vivina Rwehumbiza, amesema tathmini ya utendaji iliyofanyika imebaini kuwa idara zilizofanya vizuri zaidi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ni Idara ya Maabara, Idara ya Huduma za Dharura (Emergency Department) na Private Ward.
Alisema utambuzi huo ni sehemu ya mkakati wa hospitali wa kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa ubora, kuongeza motisha kwa watumishi na kuhamasisha ushindani wenye tija unaolenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Bi. Rwehumbiza aliwataka watumishi wote kuendelea kushirikiana, kuzingatia maadili ya kazi na kujituma ili hospitali iendelee kufikia viwango vya juu zaidi vya utoaji wa huduma za afya.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba, Dkt. Museleta Nyakiroto, aliwapongeza idara, vitengo na watumishi wote waliotambuliwa kwa kuonyesha weledi, uwajibikaji na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.

Dkt. Nyakiroto alisema mafanikio hayo yanapaswa kuwa chachu kwa idara na vitengo vingine kuongeza bidii na kujifunza kutoka kwa wenzao waliopata tuzo, ili hospitali iendelee kutoa huduma zenye ubora, usalama na zinazokidhi matarajio ya wananchi.
Aidha, alisisitiza kuwa Menejimenti ya Hospitali itaendelea kuweka mazingira yanayochochea utendaji bora kwa watumishi pamoja na kutambua na kuthamini mchango wa wale wanaofanya kazi kwa bidii, hatua itakayosaidia kuimarisha zaidi huduma za afya zinazotolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba.


