Ripoti mpya ya shirika linalohudumia watoto, Unicef, inaonesha kuwa idadi ya waathirika wa vitendo vya ukeketaji kidunia imefikia watu milioni 230, ikiwa ni ongezeko la asilimia 15 tangu mwaka 2015 licha ya hatua kupigwa kwenye mataifa ambayo jamii zimekuwa zikitekeleza vitendo hivi.
Kwa mujibu wa muandishi kinara wa ripoti hiyo, Claudia Coppa, amesema habari hiyo siyo nzuri kutokana na idadi kuwa kubwa zaidi kuwahi kuripotiwa, ripoti ambayo imetolewa sambamba na siku ya kimataifa ya wanawake.
Kulingana na utafiti wa nchi 31 bara la Afrika linatajwa kuongoza kuwa na idadi kubwa zaidi ya wathiriwa wa ukeketaji ikiwa na zaidi ya watu milioni 144, ikifuatiwa na Asia (milioni 80) na Mashariki Ya Kati (milioni sita).
Hata hivyo licha ya ripoti kuonesha kuna ongezeko kubwa , baadhi ya nchi zimeripoti kupungua kwa vitendo vya ukeketaji, ikiwemo Sierra Leone, Ethiopia, Burkina Faso na Kenya.
Wanaharakati sasa wanayataka mataifa kuongeza kasi hasa katika kudhibiti vitendo hivi kwa kuelimisha jamii na kutunga sheria kali dhidi ya wanaotekeleza.