Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Buriani amewataka watoa huduma za msaada wa Sheria Nchini kufanya kazi KWA weledi na kutoa haki kwa Wananchi ili kutimiza malengo ya Serikali kuhakikisha inamaliza migogoro sugu katika Jamii.
Ikumbukwe kuwa, Kampeni hiyo ipo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria na kupewa jina la ‘Mama Samia Legal Aid Campaign’ ,inalenga kutatua na kumaliza migogoro sugu Nchini hususani ya Ardhi na kuijenga Jamii upya isiyo na misuguano.

Dkt. Batilda ameyasema hayo leo April 7, 2025 wakati akifungua mafunzo kwa watoa huduma za msaada wa Sheria katika Jamii,ngazi ya Mkoa wa Tanga ambapo , wataalamu hao wa Sheria wataanza kutoa huduma za msaada wa Sheria katika viwanja vya Tangamano jijini Tanga kuanzia April 8 na kuenea katika Halmashauri zote 11 za Mkoa huo.
“Niwaombe,ninyi watoa huduma za msaada wa Sheria katika Jamii kwenye Mkoa wetu, naomba mfanye kazi kwa weledi na mtoe haki,msile Rushwa wala kufanya udanganyifu wowote,tambueni kuwa mnagusa maisha ya watu,msipotoa haki, migogoro haitoisha katika Jamii yetu,lengo la Serikali nikumaliza migogoro yote, huduma hii ni bure kabisa,basi na nyie fanyeni bure kama mlivyoelekezwa,” alisisitiza Dkt. Buriani.

Wakati huo huo, Dkt. Burian amekemea vikali vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia unaofanywa na baadhi ya Watu na kuonesha kutokufurahishwa na tabia chafu za baadhi ya Watu wazima na heshima zao kufanya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwa Watoto wakike na wakiume.
“Unaweza ukasema matukio ya udhalilishaji wa kijinsia kwa Watoto wakike na wakiume pengine yanafanywa na Vijana wavuta Bangi,kumbe hapana,unakuta mtu mzima na akili zake timamu anafanya mambo ya ajabu kabisa,hebu sisi wataalamu wa Sheria twendeni tukaisaidie Jamii,pia tusimame imara kukomesha matukio ya udhalilishaji wa kijinsia kwa Watoto wakike na wakiume katika Jamii yetu,” alisisitiza Dkt. Buriani