HUDUMA ZA KIBINGWA KUTOLEWA HOSPITALI ZA WILAYA KWA SIKU TANO KAGERA

Mkoa Kagera umepokea jumla ya Madaktari Bingwa na Ubingwa Bobezi 48 kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi katika wilaya 7 kwenye halmashauri 8 za mkoa huo, kupitia mpango wa Dkt. Samia Mentorship Programme.

Akizungumza mara baada ya kuwapokea madaktari hao, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Samwel Laizer, alisema ujio wa madaktari hao ni sehemu ya jitihada za serikali za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi, hususan wale wa maeneo ya pembezoni.

“Tumepokea madaktari bingwa na ubingwa bobezi pamoja na wauguzi 48 wa Dkt. Samia Mentorship kwa awamu ya nne. Madaktari hawa watatoa huduma katika hospitali za wilaya zote za mkoa wa Kagera,” alisema Dkt. Laizer.

Ameeleza kuwa, katika kambi zilizopita, zaidi ya wananchi 6,000 walipatiwa huduma za kibingwa, na kuongeza kuwa awamu hii inalenga kuongeza idadi hiyo kwa kuwafikia wananchi wengi zaidi.

“Lengo letu ni kusaidia wananchi kupata huduma hizi bila kulazimika kusafiri umbali mrefu, jambo linalopunguza gharama na muda. Tunawaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma katika hospitali za wilaya zilizo karibu nao,” alisisitiza.

Dkt. Patrick Kushoka, mwakilishi wa kambi hiyo kutoka Wizara ya Afya alisema madaktari hao wanatoka katika fani mbalimbali ikiwemo upasuaji, meno na kinywa, magonjwa ya akina mama na uzazi, magonjwa ya watoto, magonjwa ya ndani, magonjwa ya mkojo pamoja na usingizi na ganzi salama.

 “Tutahakikisha huduma hizi za kibingwa zinawafikia wananchi wote katika halmashauri za mkoa wa Kagera. Tunawaalika wananchi kujitokeza katika hospitali zetu za wilaya ili wapate huduma hizi muhimu ambazo zimeletwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema.

Ameongeza kuwa huduma za upasuaji mbalimbali zitafanyika moja kwa moja katika hospitali za wilaya kulingana na mahitaji yatakayotambuliwa.

Aidha, alibainisha kuwa pamoja na kutoa huduma, kambi hiyo inalenga kujengea uwezo kwa madaktari na wauguzi wa hospitali husika ili kuendeleza utoaji wa huduma hizo hata baada ya kambi hizo kumalizika.

Kambi hii ya Dkt. Samia Mentorship ni awamu ya nne, na imekuwa ikitekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za kibingwa na kuimarisha mfumo wa rufaa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *