HUDUMA MUHIMU NI LAZIMA ZIWAFIKIE WANANCHI – DKT. MWIGULU

Na Saulo Stephen – Singida.

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi kote nchini kwa mujibu wa Ilani ya CCM 2020–2025.

Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Nkokilangi na Nsusu vilivyopo wilayani Iramba Mkoani Singida kwenye Uzinduzi wa Mradi wa  Maji Nsusu ambao unakwenda kuwasaidia wananchi wa vijiji hivyo kuondokana na adha ya ukosefu wa maji ambayo imekuwa ikiwakabilili kwa muda mrefu wananchi hao.

Amebainisha kuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha uongozi thabiti katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa kuboresha mazingira ya huduma za kijamii ikiwemo Barabara, Zahanati, shule ,Miradi ya Maji yote hiyo ikiwa ni kwa manufaa ya Taifa.

Aidha, Dkt. Nchemba ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali katika jitihada zake za kuwaletea maendeleo huku akilaani vikali vitendo vya uchochezi vinavyolenga kuvuruga umoja ndani ya taifa.

Kwa Upande wao Wakazi wa kijiji hicho wameishukuru Serikali kwa kuwafuta machozi na kusema kuwa sasa matumaini yamerudi katika upatikanaji wa huduma ya Maji Safi na Salama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *