Na Pascal Tuliano – Tabora.
Miundombinu ni nyenzo muhimu katika ujenzi na ukuaji wa uchumi katika jamii na matengenezo ya miundombinu hiyo ni jinsi tunavyohakikisha ubora wa nyenzo hizo unaendelea kuimarika, ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi au uzalishaji.
Mwishoni mwa Septemba, Jambo Fm ilipita katika mtaa wa Ikunji, kata ya Mwinyi Manispaa ya Tabora na kujionea baadhi ya Nyaya za umeme zikiwa zimelegea kiasi ambacho mtu yeyote anaweza kuzifikia na kuzigusa, hali inayohatarisha usalama wa wapita njia na wakazi wa eneo hilo hususani watoto wadogo wanaocheza maeneo hayo.
Baadhi ya wakazi wa mtaa huo wa Ikunji waliiambia Jambo Fm namna ambavyo Nyaya hizo zinawapa hofu juu ya usalama wao pamoja na watoto wadogo.

“Kiukweli hizi Nyaya ni hatari sana kwasababu watoto wetu wanacheza haya maeneo, tunawaomba viongozi mtusaidie kutatua hili suala, tunaishi kwa wasiwasi hasa Hawa watoto wetu.” Amesema Loveness William, mkazi wa mtaa wa Ikunji.
“Ni kweli hizi Nyaya zimelegea kama unavyoona ndugu mwandishi wa habari, hii ni hatari sana na tumejaribu kuwasiliana na viongozi akiwemo diwani lakini tangu tumpe hii taarifa zaidi ya mara mbili, aliahidi kulitatua lakini hadi leo hakuna kilichofanyika.” Amesema Kadala Mohamed, mkazi wa Ikunji, manispaa ya Tabora.
Katika kutafuta ufumbuzi sa suala hili, Jambo Fm ikalazimika kubisha hodi katika ofisi za Shirika la umeme Tanzania TANESCO mkoa wa Tabora, na kufanikiwa kukutana na Afisa uhusiano huduma kwa wateja TANESCO mkoani hapa ndugu Said Mremi, ambapo amekiri kuwepo kwa changamoto za namna hiyo katika baadhi ya mitaa ndani ya manispaa ya Tabora.

“Ni kweli Kuna baadhi ya maeneo ambayo yanaripotiwa na wateja wetu kwamba nyaya zipo chini. Lakini kwa yale maeneo yanayoripotiwa kwa uharaka mafundi wetu hufika kwa wakati muafaka ili kufanya matengenezo.” Amesema Saidi Mremi.
Saidi Mremi anaongeza kuwa wananchi wanapaswa kutoa taarifa mapema pindi wanapoona hitilafu katika miundombinu ya umeme.
“Wafanyakazi wa TANESCO hawawezi kuwa kila sehemu na kujua Kila tatizo linalotokea, hivyo ni vyema wananchi muwe mnatoa taarifa TANESCO kupitia namba ya dharura ambayo ni 180 bure ili kuweza kutatua hizo changamoto.” Amesisitiza ndugu Mremi.
Baada ya kutoa taarifa hiyo, mapema wiki hii Jambo Fm imeshuhudia nyaya hizo zikifanyiwa matengenezo na TANESCO, hivyo kurejesha hali ya usalama kwa wakazi wa mtaa wa Ikunji, kata ya Mwinyi, manispaa ya Tabora.


