Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imeanza mradi wa uzalishaji wa hewa ya Oxgen hatua ambayo itaondoa adha iliyokuwa ikiipata hospitali hiyo ya kwenda kutafuta gesi hiyo katika hospitali ya rufaa kanda ya Bugando pindi wanapokuwa na wagonjwa wenye uhitaji wa huduma hiyo.
Akizungumzia mradi huo Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dr. Luzila John amesema mahitaji ya hewa ya oxgeni katika hospitali hiyo kwa ajili ya wagonjwa ni mitungi kumi kwa siku,na hospitali hiyo inazalisha mitungi 20 kwa siku hivyo uzalishaji huo umeweza kumudu mahitaji na mitungi inayosalia wanahudumia hospital za manispaa ya Shinyanga na Kahama.
Akikagua mradi huo mkuu wa mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme amesema hayo ni matokeo ya maboresho katika sekta ya afya yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita huku akisema historia imeandikwa kwani ni mara ya kwanza hewa ya oxgen kuzalishwa hospitalini hapo na kutolewa kwa wananchi bure.
Nao baadhi ya wananchi waliofika hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu wameseme uzalishaji wa hewa ya Oxgen utawasidia hususani kwa watoto njiti kwani zamani walikuwa wakilipia gharama za hewa hiyo shilingi 60,000 kwa mtungi lakini baada ya uzalishaji huo huduma hiyo kwa sasa inatolewa bure hospitalini hapo.