KIUNGO wa Azam FC Feisal Salum ameendelea kuonyesha ubora aliokuwa nao msimu uliopita ambapo hadi sasa kiungo huyo anaongoza msimamo wa kutoa pasi nyingi zilizozaa mabao (9).
Feisal hadi sasa ameongeza pasi mbili za mabao zaidi ya alizimaliza nazo msimu uliopita ambapo alitoa pasi saba huku kinara akiibuka Kipre Junior aliyekuwa akicheza timu moja na Feisal.
Jean Ahoua wa Simba anamfuatia Feisal kwa karibu akiwa nazo tano sawa na winga wa Fountain Gate Salum Kihimbwa.
Ki Aziz, Pacome Zouzoua na Clement Mzize wa timu ya Yanga wanafuatia wakiwa na pasi nne kila mmoja sawa na Josephat Arthur Bada wa Singida Black Stars mwenye pasi nne pia.
Ligi Kuu ya NBC inatarajiwa kurejea Machi, 2025 kushuhudia namna vita hii ya kupika mabao itakavyokamilika ikipisha michuano ya CHAN inayoandaliwa Tanzania.