Na Gideone Gregory,Dodoma
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti ametoa wito kwa viongozi wa mkoa wa Mara na Wilaya ya Tarime kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha matumizi ya mnada wa mpakani wa Magena.
Mhe. Mnyeti ametoa wito huo leo Juni 18,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Tarime Mjini Mhe. Mwita Kembaki aliyetaka kujua ni lini Serikali itajenga mnada wa mifugo magena ili wananchi waweze kuuza mifugo yao.
“Katika kuhakikisha biashara ya mifugo katika mnada wa Magene inafanyika katika mazingira yanayokubalika kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia biashara ya mifugo, mwaka 2021/2022, Wizara ilianza awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu muhimu katika mnda wa mifugo wa Magena kwa kujenga Mazizi, Vipakilio, Birika la maji la kunyweshea mifugo na sehemu ya kupumzika wafanyabiashara”,amesema.
Ameongeza kuwa awamu ya pili ya ujenzi wa mnada ambayo itahusisha ujenzi wa uzio na ofisi utafanyika kwa kadiri fedha itakavyopatikana.
Aidha, amesema kufuatia kukamilikwa kwa awamua ya kwanza ya ujenzi, mnada upo tayari kuanza kutumika ambapo Wizara imeshamteua mkuu wa mnada na kumpatia vitendea kazi muhimu ikiwemo pikipiki na mashine ya POS ya kukusanya maduhuli.
“Wizara inaendelea na uhamasishaji wa wananchi kutumia mnada wa Magena ili lengo la ujenzi wa mnada liweze kutimia”,amesema.