HALMASHAURI, WAZAZI MWANZA KISHIRIKIANA KUKOMESHA WIMBI LA WATOTO WA MTAANI

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana ameziagiza Halmashauri zote za mkoa huo  kushirikiana na wazazi kusimamia malezi ya watoto wao, ili kukomesha kukithiri kwa watoto wa mtaani ndani ya Mkoa huo.

Balandya ameyasema hayo hii leo wakati wa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Kamati ya mpango kazi wa Taifa wa miaka Mitano wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) pamoja na kukomesha watoto waishio mtaani.

Amesema, Halmashauri zinapaswa kuwachukulia hatua wazazi wanaokiuka sheria na taratibu za malezi ya watoto ili kujenga taifa bora hivyo ni lazima kwa pamoja Jamii kukemea matendo yanayopelekea uwepo wa watoto wa mtaani.

“Watoto ni zao la wazazi hivyo wanapaswa kushirikiana kuwalea kwa njia iwapasayo ambayo watakua nayo hadi uzeeni. Hivyo natoa wito kwa wazazi kuzingatia hilo kwani hata dini zinataka walelewe na kuwatunza katika njia ipasayo,” amebainisha Balandya.

Aidha, amesema Wataalamu wote wa ngazi za chini kwenye vijiji na mitaa mathalani Waptendaji wanatakiwa kuchukua hatua kudhibiti watoto wanaoingia mtaani kwa kuzuia kupewa pesa badala yake kuandaa utaratibu maalumu wa kuwafikia wenye uhitaji.

Kadhalika, amewapongeza maafisa Maendeleo na Ustawi wa jamii kwa kuwatambua watoto 2380 na kuwaunganisha na vituo vya malezi kwa kipindi cha 2024 na kuwaondoa 350 kwenye kazi za mtaani na kuwaunganisha na mafunzo maalumu.

Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Silas Wambura amebainisha kuwa Mkoa wa Mwanza umejidhatiti kukomesha kadhia ya watoto wa Mtaani pamoja na Ukatili wa kundi hilo na wanawake kwa kujikita kwenye usimamizi wa afua mbalimbali.

“Kuanzia januari hadi Juni 2025 Mkoa wa Mwanza umesajili vituo 85 vya malezi ya watoto wenye umri chini ya miaka 5 vikiwemo vituo 30 vinavyosimamiwa na Ilemela na Nyamagana,” amesema Dkt. Wambura.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *