HALMASHAURI MWANZA ZATAKIWA KUUSIMAMIA MRADI WA KUPAMBANA NA SELIMUNDU

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza (RAS), Elikana Balandya amewataka viongozi wa halmashauri za mkoa huo zinazopokea mradi wa kupambana na Selimundu (SCALE Care) kuusimamia vyema, kuufanya uwe sehemu ya majukumu yao ya kazi na kuhakikisha unatekelezwa kwa ufanisi ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

Balandya ametoa maagizo hayo jijini Mwanza wakati akizungumza na baadhi ya Waganga Wakuu wa halmashauri za Ukerewe, Ilemela, Nyamagana, Sengerema na Misungwi katika hafla ya kufungua mradi wa kupambana na Selimundu mkoani Mwanza – ‘Sickle Cell Access and Life Long Care (SCALE Care)’.

Amesema ugonjwa huo umeonekana kuwa tatizo kwa mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla, ambapo kati ya watoto 11,000 hadi 14,000 wanazaliwa kila mwaka nchini Tanzania wakiwa na Selimundu, kati ya hao watoto 1,730 wanatoka mkoa wa Mwanza, jambo ambalo limechochea wizara na Ofisi ya Rais Tamisemi kuanza utekelezaji wa mradi huo mkoani humo.

Amepongeza kuanzishwa kwa mradi huo unaolenga kubadilisha hali hiyo kwa kuingiza huduma muhimu kama upimaji, matibabu na huduma kinga ni hatua kubwa ya kupambana na ugonjwa huo huku lengo likiwa ni kuhakikisha hakuna motto atakayeachwa afe kwa ugonjwa wa Selimundu.

 “Nazitaka mamlaka za Serikali za mitaa ambazo ni halmashauri zote zitakazofikiwa na mradi huu kutoa ushirikiano ili huduma zitolewe kikamilifu kuhakikisha hakuna mtoto atakayeachwa na kupoteza maisha,” amesema Balandya

Katibu huyo amewataka watendaji wa afya kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya majukumu ya kazi yao ya kila siku ili mradi utakapofika mwisho matokeo yake yaendelee kwa miaka ijayo kwani shughuli ya kupambana na Sellimundu ni jumuishi.

“Utekelezaji wa mradi huu uwe sehemu ya maisha yetu ya kazi kwa sababu mradi utafika mwisho kwahiyo utakapofika mwisho matokeo yake yaendelee kwa miaka ijayo, lazima tuuingize kwenye majukumu yetu ya kila siku ili ulete matokeo endelevu,” amesema RAS Balandya.

Ameongeza kuwa; “Isionekane shughuli za mradi ni nje ya shughuli zetu, kwahiyo watendaji tutambue kwamba mradi huu ni wetu na shughuli ya kupambana na Selimundu ni jukumu letu sote.”

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Jesca Leba amesema ili kujiepusha na ugonjwa huo wananchi kujikinga na Malaria, kuanza kliniki mapema, wenzi kupima Selimundu kabla hawajafunga ndoa kuepusha kueneza ugonjwa huo kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.

“Maelekezo yote ambayo umeyatoa (RAS) tumeyachukua kwa ajili ya utekelezaji. Asilimia 90 ya watoto huwa hawafikishi miaka mitano, Kanda ya Ziwa imeathiriwa zaidi kwa sababu imekuwa na kiwango kikubwa cha Malaria,” amesema Dkt. Leba

Akizungumzia mradi huo, Mkufunzi Mwandamizi Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Dkt. Lulu Chirande amesema amesema kupitia mradi huo watafanya upimaji wa Selimundu kwa watooto wachanga ili kugundulika mapema na kupata matibabu kwani kufanya hivyo kutasaidia kwa asilimia kubwa kupunguza tatizo hilo.

Dk Chirande ambaye ni Daktari bobevu wa magonjwa ya damu na saratani kwa watoto, amesisitiza kuwa takribani watoto 500,000 duniani huzaliwa wakiwa na Selimundu huku asilimia 75 wakitoka kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania, ambapo Tanzania ni ya tano ulimwenguni na ya nne Afrika kwa wingi wa wagonjwa wa Selimundu na asilimia saba ya vifo kwa watoto chini ya umri wa miaka saba inatokana na ugonjwa huo.

“Tutafanya ngazi ya jamii na vituo vya afya tukishirikisha jamii kupitia uelimishaji, kufanya vipimo, kushirikiana katika huduma za chanjo zinazoendelea, kuwawezesha na kuwajengea uwezo watoa huduma katika vituo vya afya ili watoe huduma kwa ufanisi na kwa ufasaha,” amesema Dk Chirande na kuongeza.

Kwa upande wake, Mratibu huduma za Selimundu Wizara ya Afya, Dkt. Asteria Mpoto amesema watendaji wote waliopata mafunzo ya namna ya kutekeleza mradi huo yaliyoendeshwa kwa siku tatu wanapaswa kutekeleza majukumu yaliyokusudiwa kuliko kurudi vituoni na kupangiwa majukumu mengine, jambo ambalo litakwamisha ufanisi wa mradi huo.

“Mikakati ya wizara kupambana na Selimundu ni kupima watoto wanapozaliwa ili kugundua mapema na kuanza matibabu, pia kutoa elimu kwa vijana kuhusu Selimundu ili wasije wakaoana na kusababisha tatizo liendelee kuwa kubwa,” amesema Dk Mpoto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *