Katika kuendana na mabadiliko ya Mitaala ya Elimu ya Msingi na Awali, Halmashauri ya Wilaya ya Magu imegawa zana za ufundishaji na ujifunzaji zenye thamani ya Sh milioni 34 kwa shule za msingi 53 za serikali zenye madarasa ya awali wilayani humo.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa zana hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mohamed Ramadhani amewataka walimu wa shule zilizopokea zana hizo kuzitumia vizuri ili ziweze kuleta matokeo chanya kwa Wanafunzi.

“Kwa hiyo mwalimu jitahidi hiki ambacho utakipokea kahakikishe kinaenda kuingia kwenye uelewa wa mtoto, kisiende kufungiwa staff… badala ya kufungiwa stoo ili visipotee, wafundisheni watoto namna ya kuvitumia na kuvitunza ili wasiviharibu kwa sababu pamoja na utundu wao wana uelewa hivyo nina uhakika watavitunza,” amesema.
Katika hatua nyingine Mohamed amesema kupitia zoezi la utoaji w zana hizo anamini itakwenda kuongeza chachu kwa watoto kujifunza na matumaini yake ni kuona mabadiliko kwa siku za baadae.

“Mwaka juzi tulitoa kwa shule 28, mwaka huu tumetoa kwa shule 53 lakini Magu tuna shule 111 za serikali, sasa ifike mahali mtoto wa chekechea anayetoka palipo na zana hizi awe na utofauti lakini naamini pia wasiopata wataenda kuiga mfano huu kuzitengeneza kwa wingi zaidi.
Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi katika wilaya ya Magu Mwalimu Jackson Buhatwa amesema zana hizo zimetengenezwa kwa ufadhili wa mradi wa BOOST na kwa awamu hii ni shule 53 ndio zitanufaika na zana hizo.

“Tuna jumla ya shule 111 za serikali lakini awamu hii ya pili ni shule 53 zimefaidika na mradi huu. Kila shule imepata Sh 6045,500 kwa ajili ya utengenezaji wa zana ambazo zitatumika kufundishia wanafunzi wa awali.
Nao baadhi ya walimu kutoka katika shule zilizopokea zana hizo wamesema zitakwenda kuwasaidia watoto kupata uelewa zaidi, huku zikienda kuwafanya waipende shule zaidi.

“Kutokana na mabadiliko ya mitaala zana hizi zitasaidia sana makuzi ya mtoto kuendana na wakati. Tunaahidi kufanya kazi kwa bidi lakini pia zana zitatumika ipasavyo kwa watoto, tutaenda kusimamia badala ya kuwa kama pambo,” amesema mwalimu Daniel Joseph
“Tulikuwa na changamoto nyingi kuhusu zana za ufundishaji kwa sababu mwanafunzi ilikuwa haoni zaidi ya kile kinachoandikwa ubaoni lakini sasa ataona na watoto watapokea maarifa, tunaahidi tutafanya juhudi ili watoto waende kupokea maarifa kupitia vifaa hivi,” amesema mwalimu Marry Shigela.