Na Tryphone Odace, Kibondo Kigoma.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amezitaka Halmashauri mkoani humo kuendelea kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha zinazotumika.
Balozi Sirro ametoa agizo hilo leo Agost 21 akiwa wilayani Kibondo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayotarajiwa kukaguliwa wakati wa mbio za Mwenge wa uhuru zitakazofanyika Mkoani Kigoma mwezi Septemba 2026.

Alisema Serikali na wananchi wanatarajia kuona miradi ya maendeleo ikitekelezwa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa, huku wahusika wakihakikisha miradi inakamilika kwa wakati na inakuwa na tija kwa wananchi.
“Matarajio ya Serikali pamoja na wananchi ni kuona miradi ikitekelezwa katika viwango vinavyotarajiwa na kukamilika kwa wakati,” alisema Balozi Sirro.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kwa kuonesha usimamizi mzuri na madhubuti wa miradi ya maendeleo, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kila mradi unatekelezwa kwa kuzingatia thamani yake na manufaa yanayotarajiwa kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Kanali Mstaafu Aggrey Magwaza, amesema halmashauri itazingatia ushauri na maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na kuhakikisha maeneo yenye mapungufu yanafanyiwa kazi ili kuboresha utekelezaji wa miradi.

Alisema hatua hiyo ni sehemu ya kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa wilayani Kibondo inakidhi viwango vinavyotakiwa na inatoa huduma stahiki kwa wananchi.


