HAKUNA MGOGORO WA MPAKA KATI YA KALIUA NA KAHAMA – TAMISEMI.

Na Gideon Gregory, Dodoma 

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zainabu Katimba amesema kwa mujibu wa Tafsiri ya ardhi ya Matangazo ya Serikali ya uanzishwaji wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga na Kaliua Mkoani Tabora hakuna mgogoro wa mpaka kati ya mikoa hiyo miwili. 

Mhe. Katimba ameyasema hayo leo Mei 6, 2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani aliyehoji ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka wa Shinyanga na Tabora katika eneo la Ushetu na Kaliua ambao umechukua muda mrefu.

“Mgogoro uliopo wa mpaka ni kati ya Hifadhi ya Msitu wa Mto Igombe unaomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na msitu wa Hifadhi wa Ushetu Ubagwe unaomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu,”amesema. 

Adha, ameongeza kuwa mgogoro huo umetokana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)  kuweka alama za mipaka kwenye eneo la Hifadhi ya Msitu wa Ushetu Ubagwe uliopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Mkoani Shinyanga. 

“Hata hivyo, kwa mujibu wa Matangazo ya Serikali ya uanzishwaji wa Hifadhi ya Msitu wa Igombe river, Tangazo la Serikali Namba 32 la mwaka 1958  na Hifadhi ya msitu wa Ushetu Ubagwe, Tangazo la Serikali na 442 la mwaka 1958 hakuna mwingiliano wa mipaka kati ya Hifadhi hizi mbili “ameongeza. 

Amesema Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) itaendelea kuhakikisha Hifadhi ya Msitu wa Igombe river inabakia kwenye mipaka yake kama ilivyo kwenye Tangazo la Serikali Namba 32 la mwaka 1958  la uanzishwaji wa Hifadhi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *