HAKUNA FOMU MOJA YA KUGOMBEA UBUNGE – NCHIMBI.

Na Gideon Gregory,  Dodoma. 

Katibu Mkuu wa chama cha mapinduzi CCM Taifa Dkt.Emanuel Nchimbi amewataka wabunge wa chama hicho kuacha mara moja tabia ya kupitisha fomu moja ya wanachama ili wawe wagombea pekee katika majimbo yao kwani chama hiyo kitawaengua pindi zoezi la kupitisha wagombea litakapo anza.

Dkt. Nchimbi ameyasema hayo leo Februari 19,2025 Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa  mafunzo ya Watendaji wa Kata na Makatibu Tawi wa Mkoa wa Dodoma ambapo amesema kuwa tabia hiyo imekuwa ikionekana mara kwa mara kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

“Lakini vilevile vimeanza vikao vya matamko kupitia mikutano mikuu, Halmashauri kuu kutoa tamko baada ya utekelezaji wa mbunge wetu au diwani wetu apite bila kupingwa sasa nawatumia salamu kuwa kitu hicho hakipo na kadri unavyozidi hamasisha matamko katika jimbo/kata yako ndivyo tutakuengua kwa urahisi” amesema Dkt.Nchimbi.

Aidha ameongeza kuwa kumekuwepo na utaratibu kwa watu wanaotamani kuwa wagombea kutengeneza matukio mbalimbali katika maeneo kama kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha bibi/babu na kisha kuwaalika wajumbe zaidi ya 1,000 na kuwalipa posho ambapo amesema kuwa chama hicho kinaendelea kuwafuatilia.

Pia amewasisitiza madiwani na wabunge walioko madarakani kuacha kupuuza majukumu yao kwa kisingizio cha maandalizi ya uchaguzi, akisema chama kitafanya tathmini kwa kila mgombea kulingana na utendaji wake, si kwa uwezo wa kutoa fedha kwa wapiga kura.

“Tumeshuhudia watu wakichaguliwa lakini wanakaa miaka mitano bila kufanya kazi kwa sababu wanajua wapiga kura wachache wa ndani ya chama watakaowarudisha tena madarakani. Mfumo wetu mpya unalenga kumchagua mgombea kwa misingi ya kazi zake, si kwa kutumia rushwa au mbinu za kificho. Tunataka ukichaguliwa ukafanye kazi kwa wananchi,” amesisitiza. 

Wakati huo huo ameeleza kuwa mabadiliko ya Katiba ya CCM yaliyofanyika chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yalilenga kuongeza idadi ya wapiga kura katika kura za maoni ili kupata taswira pana ya maoni ya wananchi na kudhibiti mianya ya rushwa.

Amesema kuwa chama hicho kinahitaji kuwa na wanachama wenye umoja na kuweza kukijenga chama hicho na siyo vinginevyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *