HAKUNA ANAYEWEZA KUZUIA UCHAGUZI MKUU WA 2025 – NCHIMBI

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesisitiza kuwa hakuna raia yoyote mwenye mamlaka ya kuzuia uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo Wananchi watapiga kura kuchagua Madiwani, Wabunge na Rais.

Amesema kuwa uchaguzi huo ni takwa la kisheria, na hakuna mtu au chama cha siasa kinachoweza kuingilia au kuzuia mchakato huu wa kidemokrasia.

Balozi Nchimbi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari akiwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu Maalumu ulioandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), linalojiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, na wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa jukwaa hilo, utakaofanyika Aprili 5, 2025.

Katika hotuba yake, Dk. Nchimbi pia alizungumzia kauli ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambalo limekuwa likisisitiza kwa muda mrefu misimamo yake ya “no Reforms, no Election”, akisema kuwa jitihada hizo hazitaweza kufanikiwa.

Amesema, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna chama cha siasa wala kiongozi wa serikali anayeweza kusitisha uchaguzi mkuu. Aliendelea kusema kuwa, ingawa CHADEMA wanahaki ya kutoshiriki uchaguzi, hawawezi kuzuia wengine kushiriki au kufanya uchaguzi.

“Kwa mujibu wa sheria, uchaguzi ni haki ya kikatiba ambayo inatakiwa ifanyike. Hivyo, hakuna mtu anayeweza kuingilia zoezi hili. Kama kuna chama kinachojisikia haliko tayari, kinaweza kuchagua kutoshiriki uchaguzi, lakini kuzuia uchaguzi huo, hilo ni jambo lisiloweza kutokea,” alisema Balozi Nchimbi.

Aidha, aliwataka wananchi kuepuka kushinikiza vyama vya siasa visivyotaka kugombea katika uchaguzi huu, akisisitiza kuwa CHADEMA wanaweza kuamua kutoshiriki uchaguzi wa mwaka huu na badala yake watapata nafasi nyingine kwenye chaguzi zijazo, kama vile za mwaka 2030 au 2035.

Hata hivyo, aliongeza kuwa, licha ya vyama vya siasa kuwa na haki ya kutoshiriki, wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi na kutumia haki yao ya kupiga kura, ili kuchagua viongozi watakao jitosheleza kwa nafasi mbalimbali za uongozi.

Aidha Nchimbi amesema kuwa, uchaguzi wa mwaka 2025 utaendelea kama ilivyopangwa, na kuwa ni kipaumbele cha taifa kuhakikisha kuwa mchakato huu wa kidemokrasia unatekelezwa kwa kuzingatia sheria na haki za kila mmoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *