HAIKUBALIKI: UKEKETAJI KAA LA MOTO KWA WANAWAKE, WATOTO

Na  Alphonce Kaji – Jambo Media.

Ukeketaji kwa Wanawake na Watoto bado ni changamoto kubwa katika kijamii na ya kiutamaduni nchini, ambayo inaendelea kuathiri maelfu ya Watendewa.

Kitendo hiki, ni ukiukwaji wa haki za binadamu na kinaendelea kujitokeza katika baadhi ya jamii kutokana na Imani, mila na desturi zilizokita mizizi kwa muda mrefu ikiwa ni kuondoa kwa kiungo au viungo vyote vya nje ya uzazi wa mwanamke au mtoto wa kike na hivyo huumiza kiungo hicho kwa sababu zisizo za kitabibu.

Shirika la Afya Duniani (WHO), lina ainisha ukeketaji katika aina nne, na kuweka wazi Kitendo hiki hakina faida zozote za kitabibu na kinatambuliwa duniani kote kama ni ukatili wa kijinsia.

Takwimu za Shirika hilo za mwaka 2021 zinaonesha viwango vya juu sana za ukeketaji    katika nchi kama Somalia 98% Guinea 97% na Misri 87%.

Mpaka kufikia mwaka 2024, inakadiriwa kuwa zaidi ya wanawake na watoto wa kike milioni 230 duniani kote wamepitia ukeketaji, ongezeko la karibu takribani asilimia 15 tangu mwaka 2016.

Katika takwimu hizo bara la Afrika linaendelea kubeba mzigo mkubwa zaidi, likiwa na takribani visa milioni 144, likifuatiwa na Asia yenye visa takribani milioni 80 na Mashariki ya Kati ikiwa na visa milioni 6.

Pamoja na changamoto hizi, mafanikio yameonekana katika baadhi ya nchi za Afrika, ikiwemo Ethiopia, Kenya na Tanzania, ambako viwango vya ukeketaji vimepungua kwa zaidi ya asilimia 30 katika miongo ya hivi karibuni.

Kwa mujibu wa takwimu za UNICEF za mwaka 2024, Afrika inaendelea kuwa na idadi kubwa zaidi ya manusura wa ukeketaji duniani,huku Tanzania zimeonesha maendeleo ya kupunguza kiwango cha ukeketaji katika kipindi cha miaka ya karibuni.

Nchini Tanzania, ukeketaji bado ni suala nyeti linalohitaji hatua za kimkakati Kwa mujibu wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa Mwaka 2022 (TDHS-MIS), kiwango cha kitaifa cha ukeketaji kwa wanawake wenye umri wa miaka 15 – 49 ni asilimia 8, ikiwa ni pungufu kidogo ikilinganishwa na tafiti za awali.

Lakini mikoa ya Arusha na Manyara inatajwa bado kuwa kinara wa ukeketaji nchini ikiwa 43% huku mkoa wa Mara uliokua kinara wa visa vya ukekektaji nchini ukishuka hadi asilimia 28

Ukeketaji unajitokeza zaidi miongoni mwa jamii za Wamasai, Wakurya, Wanyaturu, Wairaqw, Warangi na Wagogo na kwa kiasi kikubwa hufanywa na wazee wa kimila kwa kushirikiana na mangariba kwa kutumia zana za jadi.

Hata hivyo, mapambano dhidi ya ukeketaji yanakumbwa na changamoto za imani za jadi zilizojengeka kwa muda mrefu, pamoja na upungufu wa rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa sheria na elimu kwa umma. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima ameweka wazi mashaka yake juu watendao vitendo hivyo kuwa na tatizo la afya ya akili.

Wanaume wanatajwa kuhusika kukwamisha jitihada hizo kwa kiwango kikubwa wakidaiwa kukataa kuoa wanawake ambao hawajakeketwa.

Katika kuimarisha mapambano dhidi ya ukeketaji serikali imezindua mkakati wa taifa wa kisekta wa kutokomeza ukeketaji nchini ukiwapa kipaumbele wanaume katika harakati hizo

Nchini Tanzania, ukeketaji ni kosa la jinai kwa mujibu wa Kifungu cha 160 (1) na (2) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Toleo lililofanyiwa Marejeo la mwaka 2025. Adhabu kwa mkosaji ni faini isiyopungua shilingi milioni mbili za Kitanzania, kifungo cha miaka mitano hadi kumi na tano au adhabu zote kwa pamoja, ambapo pia Mahakama pia inaweza kuamuru fidia kwa aliyeathiriwa.

Picha Credit@ vyanzo mbalimbali vya mitandao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *