Jeshi la polisi Mkoani Tabora limesema kuwa hali ya amani na utulivu iliyopo mkoani humo imetokana na ushirikiano uliopo kati yao na wananchi.
Kamanda wa Polisi Mkoani Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Richard Abwao ameyasema hayo wakati wa Uzinduzi rasmi wa Gridi ya Nishati ya MAISHA FRESH Mboka Manyema Tabora, akidai ulinzi shirikishi kupitia sungusungu imekuwa chachu ya kuboresha hali ya utulivu na usalama.
SACP Abwao ameongeza kuwa, kumekuwa na jitihada za makusudi za kutoa elimu kwa wananchi ndani ya jamii kupitia Sungusungu na kwamba Polisi imekuwa likishirikiana na wananchi kupitia michezo jambo ambalo limechangia kuimarisha uhusiano mzuri kwa jamii.

Katika hatua nyingine Jambo Fm imezungumza na Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Tabora na kueleza furaha waliyonayo baada ya ujio wa Gridi hii ya MAISHA FRESH yenye ujazo wa Megawati 99.7, na kuomba kuongezewa dozi ya burudani na vipindi vya hamasa kwa vijana.
Jambo media group imeendelea na kampeni yake ya kuunganisha gridi ya umeme wa nishati ya MAISHA FRESH katika mikoa yote 11 inayopatikana kanda ya ziwa, ikiwa na Lengo la kuwaunganisha wakazi wa ukanda huu katika gridi moja ya Maisha Fresh.