Mkazi wa Mtaa wa Kota, Kata ya Mlandege Mkoani Iringa, Goodluck Mgovano aliyekadiriwa kuwa na umri wa miaka 33 anadaiwa kumuua Mtoto wake Alvini Mgovano mwenye umri wa miaka minne kwa kumnyonga na kamba ya viatu huku akijirekodi kwa simu yake ya mkononi wakati akimnyonga Mtoto na alipomaliza akapiga selfie na mwili wa Mtoto na kuacha ujumbe ulioelekeza wapi Mtoto huyo azikiwe.
Ndugu na Majirani wamesema wakati Baba anamnyonga Mtoto, Mkewe hakuwepo nyumbani na aliporudi alipiga kelele ‘Mume wangu amempa Mtoto sumu’ ndipo Majirani waliingia ndani na kukuta Mtoto amelala kitandani, walimpa maziwa lakini yalikuwa hayapiti ndipo ikabainika amefariki.
Mtuhumiwa aliacha ujumbe uliosema “Chanzo cha mauaji haya ni ugomvi uliotokea kati yangu Mimi na Mke wangu mnamo October 6 , 2023 na Mimi naenda kujiua na nataka Mimi na Mwanangu tuzikwe Kijiji cha Itendulinyi”
Diwani wa Kata ya Mlandege, Jackson Chaula amesema Mtuhumiwa alikuwa anafanya kazi ya ubebaji mizigo katika magari lakini hakuwa na shida yoyote.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa Alfred Mwakalebela amekiri kupokea mwili huo na kusema mwili huo ulikuwa na makovu ya shingoni.