GEITA: WANAFUNZI 120 KUSHIRIKI MICHEZO YA UMITASHUMTA KITAIFA MKOANI IRINGA

Frank Aman – Geita.

Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati ameagana rasmi na timu ya wanafunzi 120 Kutoka Mkoa wa Geita ambao watashiriki Mashindano ya UMITASHUMTA Ngazi ya Taifa Mkoani Iringa.

Akizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo kwa ngazi ya Mkoa katika viwanja vya shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu Manispaa ya Geita, Katibu Tawala Mkoa wa Geita amewapongeza washiriki wote kwa kufanya vyema katika michezo ya aina mbalimbali.

 “Isingekuwa utaratibu ,wote mmefanya vizuri, lakini muongozo unaelekeza Mkoa kwenda na wanafunzi 120 pekee hivyo hatuna budi kupeleka timu yenye idadi ya wanafunzi waliokusudiwa.”ameongeza Gombati 

Gombati ametoa rai kwa wanafunzi waliokosa nafasi ya kwenda kushiriki UMITASHUMTA ngazi ya Taifa kuto kata tamaa na waendelee kujituma na Kufanya maandalizi ili mwakani panapo majaaliwa wawepo kwenye timu ya Mkoa itayoshiriki mashindano ya kitaifa. 

Pia amewaasa wanafunzi waliopata nafasi ya kushiriki mashindano ya kitaifa kuwa na nidhamu,bidii na ubunifu ili warudi na vikombe vya ushindi.

Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Geita Antony Mtweve, amesema timu ya Mkoa yenye wanafunzi 120 pamoja na itaanza safari ya kuelekea Mkoani Iringa tarehe 5 Juni 2025 ambapo mashindano ya Kitaifa yatafanyika huko.

Afisa Michezo Mkoa Bahati Rodgers, amesema wanafunzi 120 wanaoenda kushiriki mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya taifa wamepatikana ndani ya halmashauri  6 zote za Mkoa wa Geita, ambao wanashiriki kwenye michezo ya mpira wa miguu kwa wavulana na wasichana,mchezo wa wavu,kikapu ,riadha pamoja na fani za ndani na watawakilisha Mkoa wa Geita kitaifa kwa michezo hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *