Na Ibrahim Rojala – Geita.
Changamoto ya ukosefu wa huduma ya uhakika ya chakula shuleni imetajwa kuathiri ufanisi wa wanafunzi wawapo masomoni kwa baadhi ya shule zilizopo katika kata ya Butobela wilayani Geita mkoani Geita.
Afisa Elimu kata ya Butobela, Ndio John Otieno ameeleza hayo akiwa katika shule ya msingi Bagaza yenye jumla ya wanafunzi 1,757 baada ya kushuhudia zoezi la upokeaji wa mahindi gunia 30 na Sukari Kilo 250 kutoka Taasisi ya Mapung’o Foundation ambapo amesema msaada huo utakwenda kuondoa changamoto ya huduma ya chakula katika shule hiyo.

Ameongeza kuwa huduma ya uhakika ya upatikanaji wa chakula itasaidia kupunguza changamoto za wanafunzi kukosa utulivu wakati wa masomo, utoro uliokuwa ukisababishwa na wanafunzi kukosa huduma ya chakula,hali itakayosaidia kuongeza kiwango cha ufaulu katika shule hiyo.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bagaza, Damas Madata amesema msaada huo utatatua changamoto ya upatikanji wa chakula,kuongeza idadi ya mahudhurio ya wanafunzi madarasani pamoja waalimu kutanua wigo mzuri wa kufundisha wanafunzi walio na utayari darasani.

“Tunishukuru Taasisi ya Mapung’o Foundation kwa msaada huu,waendelee kufanya hivi ili jamii iendelee kunufaika na kupata maendeleo zaidi na zaidi”ameeleza Mwalimu Madata
Baadhi ya wanafunzi wanaotarajiwa kunufaika na chakula hicho,wameishukuru Mpung’o Foundation na kueleza kuwa msaada huo utawasaidia kusoma kwa utulivu darasani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyakagwe,Daudi Lumala Hungwi ameishukuru Tasisi hiyo kwa msaada huo na kueleza kwamba umekuwa chachu ya kuongezea upungufu wa chakula uliopo kutokana na kusuasua kwa michango ya wazazi na kumshukuru diwani wa kata ya Butobela Pascal Mapung’o kwa maada wake kwa wanafunzi na kutoa wito kwa wazazi kuendela kuchangia chakula shuleni.
“Kwa kuunga mkono juhudi hizi za Diwani na Yaasisi ya Mapung’o Foundation nimetoa kilo 200 za sukari kuunganisha nguvu pale kwa Diwani na Taasisi ya Mapung’o Foundation,nadhani sasa itakuwa ni chachu kwa watoto wetu kuimarika kimasomo”amesema Daudi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mapung’o Foundation,Marko Victor ameeleza kuwa baada ya kutoa msaada huo waliungwa mkono na mwenyekiti wa seikali ya kijiji cha Nyakagwe aliyetoa kilo 200 za sukari akieleza kwamba dhamira ya taasisi hivyo ni kuleta matumaini kwa wanafunzi na kuongeza kiwango cha ufaulu.
“Taasisi ya Mapung’o ina mipango na Projects nyingi sana,lazima tuoneshe kile ambacho tunakifanya kwa jamii ili tupate wadau wengi waweze kujitolea na kuungana na sisi,hata kama hawatoungana na sisi katika eneo letu hili basi wawe na moyo wa kujitolea kama tulivyofanya”amesema Marko.


