GEITA: CHANGAMOTO ZINAZOWAKWAMISHA VIJANA KIUCHUMI ZAWEKWA HADHARANI

Na Ibrahim Rojala – Geita.

Kutozitambua fursa za kiuchumi zilizopo ndani ya Jamii, mitaji na masoko vimetajwa kuwa ni baadhi ya changamoto zinazowakabili vijana kujikwamua kiuchumi zikichochewa na  kukosekana kwa taarifa za uwepo wa fursa ambazo zinaweza kutatua changamoto hizo na kuwafanya vijana kujikwamua kiuchumi.

Hayo yameelezwa Februari 10, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela wakati akifungua kongamano la  Vijana wa halmashauri ya Manispaa ya Geita lililofanyika katika Ukumbi wa Golden Social Hall likiwakutanisha vijana kutoka katika kada mbalimbali ndani ya Manispaa ya Geita likiongozwa na malengo makuu manne ya kimkakati.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela.

Kupitia Kongamano hilo, RC Shigela amaesema kwamba ili vijana waweze kuendana na kasi ya dunia ya sasa wanapaswa kupata maarifa na matumizi sahihi ya muda,kujitambua,kufanya kazi kwa bidii,kujifunza mambo mapya pamoja na kuendeleza utamaduni wa kuyafanyia kazi  mambo ambayo wamekuwa wakijifunza hatua itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi.

“Tumepiga hatua kama Taifa kwenye masuala ya elimu,vijana wengi sasa hatuzungumzi tena suala la kuandika na kusoma,limekuwa jambo la kihistoria,tumepiga hatua katika kuendelea kupanua wigo wa fursa tulizonazo lakini changamoto yetu bado inaendelea kuwa aidha ni changamoto ya masoko,au ya mitaji au kutozijua hizo fursa zenyewe ambazo kama taifa tumzezipiga,” amesema.

Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati.

Akizungumza katika Kongamano hilo, Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati amesema watendaji wa serikali ndani ya mkoa wa Geita wataendelea kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), maono na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan na yanayotolewa na mkuu  wa Mkoa wa Geita ili kuhakikisha changamoto za vijana zinatatuliwa ndani ya mkoa huo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashim Abdallah Komba amesema kongamano hilo ni matokeo ya dhamira ya kuwakusanya vijana ndani ya wilaya ya Geita kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili,hatua ambayo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwataka viongozi kushuka katika ngazi za chini na kusikiliza changamoto zinazowakabili vijana ndani ya Jamii.

Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashim Abdallah Komba.

“Niwashukuru sana Wakurugenzi wetu wote,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita  pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Geita kwa namna ambavyo tumekubaliana pamoja kushuka chini kulifikia kundi hili la Vijana,” amesema DC Komba.

Baadhi ya vijana walioshiriki Kongamano hilo, akiwemo Aristides Oscar na Marieta Lubeja wameishukuru serikali kwa kuwakutanisha pamoja vijana wakieleza kwamba imekuwa chachu kwao katika kuzitambua na kuzitumia fursa za kiuchumi zilizopo ndani ya jamii na kuwataka vijana wengine kutumia fursa za mikopo ya asilimia 10, inayotolewa na halmshauri pamoja na kutumia mitaji midogo waliyonayo, kuanzisha shughuli za kiuchumi.

Aristides Oscar (kushoto), Marieta Lubeja (kulia).

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Yefred Edson Myenzi  ameeleza kuwa kongamano hilo limefanyika likiwa na malengo matano ambayo ni,kuwaleta vijana pamoja ili kushirikisha na kubadilishana  taarifa mbalimbali za fursa zilizopo ndani ya Manispaa,mkoa wa Geita na maeneo jirani.

Pia kubainisha fursa mbalimbali za uwezeshaji vijana kiuchumi pamoja na kuwajengea uwezo wa kujiamini na uthubutu wa kuchangamkia fursa kwa kutoogopa chochote na kujifunza kuanza na walichonacho ili kujikwamua kiuchumi.

Sehemu ya Washiriki wakifuatilia jambo katika Kongamano la Vijana wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita.

Malengo mengine ni kupambana na mitazamo hasi na kuimarisha uzalendo na Ulinzi wa Taifa Miongoni mwa vijana pamoja na kusaidia kuondoa misongo ya mawazo miongoni mwa vijana kwa kuwakutanisha pamoja ili kujadili mambo yanayowahusu.

Kongamano hilo limeandaliwa na halmashauri ya wilaya ya Geita kwa Ufadhili wa Mgodi wa dhahabu wa Geita Gold Mine Limited (GGML) na African Underground Mines na kuwakutanisha vijana zaidi ya 1300 kutoka ndani ya Manispaa ya Geita.

Vijana wameshauriwa kutumia fursa za mikopo ya asilimia 10, inayotolewa na Halmashauri kujiinua kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *