Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), limelisimisha uanachama Shirikisho la Mpira wa Miguu la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (FECOFOOT) mpaka hapo itakapotangazwa vinginevyo.
Kwa mujibu wa barua ya FIFA kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), uamuzi huo wa kuisimamisha FECOFOOT uliofanywa Februari 6, 2025 umezingatia Ibara ya 16 ya Katiba ya FIFA.

FECOFOOT imepotezahaki zote za uanachama kama zilivyoainishwa katika Ibara ya 13 ya Katiba ya FIFA, hivyo klabu za DRC hazitashiriki katika mashindano yoyote ya kimataifa mpaka hapo adhabu hiyo itakapoondolewa.
Uamuzi huo unamaanisha kuwa FECOFOOT, wanachama wake na maofisa wake hawatanufaika na programu za maendeleo, kozi au mafunzo kutoka FIFA au Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) katika kipindi hiki ambapo wanatumikia adhabu hiyo.

Pia wanachama wa FIFA pamoja wanachama wao wanakumbushwa kutokuwa na uhusiano wowote wa kimichezo na FECOFOOT au wanachama wake katika kipindi hiki ambapo FECOFOOT imesimamishwa.

FIFA imetoa adhabu hiyo kutokana na Waziri wa michezo wa Congo, Hugues Ngouélondélé kuingilia masuala ya kimichezo kwa kuvunja Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo na kuteua Kamati ya muda, ili kuhakikisha usimamizi na mwelekeo wake unakuwa na weledi.
