Na Saada Almasi – Simiyu.
Chama cha wachimba madini Tanzania FEMATA kimeazimia kufanya matembezi nchi nzima ya kuenzi miaka minne ya uongozi wa Raisi Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuishika mkono sekta hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017 hadi sasa Serikali imefanikiwa kupandisha makusanyo kutoka shilingi Bilioni 200 kwa mwaka hadi Trilioni 1.1.
Akizungumza na wachimbaji wadogo wilayani Bariadi mkoani Simiyu Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa kumekuwa na maboresho katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya madini kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi ambapo kwa sasa bado vifaa vya kisasa vya kubaini madini katika machimbo vinaendelea kuletwa sambamba na kuboresha mazingira ya kazi kwa wachimbaji hao.

“Sekta zote za kiuchumi ni sekta nyeti ambazo serikali inawekeza ili kuinua uchumi wa nchi na sekta hii ya madini tayari vifaa vya kisasa vinaletwa ambavyo vitasaidia kubaini ni wapi madini yanapatikana lakini pia mazingira mazuri ya kazi yanaendelea kuboreshwa ikiwa ni pamoja na miundombinu ya maji,barabara na umeme migodini,” Naibu Waziri Kiluswa.
Naye Raisi wa Wachimbaji Madini Nchini, John Bina amesema kuwa matembezi hayo yatafanyika nchi nzima na yanalenga kuionyesha dunia manufaa makubwa yaliyopayikana katika sekta hiyo sambamba na malengo ya kufungua soko la madini Afrika ili wawekezaji waone uwingi wa madini yanayopatikana nchini Tanzania.

“Tanzania hasa Simiyu kuna aina nyingi ya madini yanayozalishwa sasa matembezi haya hadi kufikia kilele chake mwezi Mei tunataka kuionyesha Dunia mafanikio makubwa ya wachimbaji nchini ukizingatia kwa sasa soko la madini la Afrika litafunguliwa na kila mwekezaji ataiona Tanzania,” alisema Raisi wa madini Bina.
Kwa upande wake afisa madini mkazi wa mkoa wa Simiyu Maige Makolobela amesema kuwa licha ya kutokuwa na migodi mikubwa mkoani humo bado wachimbaji wadogo wanaongoza kwa uchangiaji mzuri katika pato la Taifa ambapo hadi sasa tayari wamechangia asilimia 98 katika pato hilo.

“Sisi tuliopo hapa ni wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na akina mama wauza fero,vijana wachenjuaji kwa sababu hakuna uchimbaji mkubwa mkoani hapa lakini tunajivunia kuwa tunaongoza kwa uchangiaji wa pato la Taifa kwani hadi sasa tuna asilimia 98 bado kidogo tufike asilimia 100 za kuchangia pato la taifa,” amesema Makolobela.



