FCC YAENDELEZA USIMAMIZI USHINDANI WA HAKI, ULINZI MASLAHI YA WANANCHI

Na Gideon Gregory  – Dodoma.

Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), imesema inaendelea kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi kwa kusimamia ushindani wa haki katika biashara pamoja na kulinda maslahi ya watumiaji, hatua inayochangia pia kufungua fursa za ajira na uwekezaji kwa vijana nchini.

Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari leo Machi 05,2026 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 tume imeendelea kuruhusu miungano mbalimbali ya makampuni katika sekta tofauti za uchumi ili kuongeza uwekezaji, ushindani wa soko na ajira kwa Watanzania.

“FCC iliridhia miungano miwili ya makampuni katika sekta ya kilimo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 20.4. Miungano hiyo inahusisha kampuni ya Africado Limited na AgDevCo Limited pamoja na muungano wa Amboni Sisal Properties Limited na Amboni Spinning Mill Limited,” amesema. 

Amesema uwekezaji huo utaongeza uwezo wa uzalishaji na usindikaji wa mazao ya kilimo kama parachichi na katani huku ukiongeza ajira kwa wakulima wadogo na vijana wanaojihusisha na shughuli za kilimo.

Katika sekta ya mawasiliano, amesema FCC iliridhia ununuzi wa kampuni ya Habari Node Limited na mfuko wa uwekezaji wa Pembani Remgro Infrastructure Fund II.

Muungano huo unatarajiwa kuongeza mtaji na kuboresha huduma za intaneti nchini, hususan katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Tanga na Mara.

“Hatua hiyo itasaidia kupanua upatikanaji wa intaneti ya bei nafuu na kuimarisha shughuli za kidijitali zinazowezesha vijana kushiriki katika uchumi wa kidijitali,” amesema. 

Pia ameongeza kuwa FCC imeendelea kudhibiti uingizaji na usambazaji wa bidhaa bandia nchini ili kulinda biashara halali na watumiaji. Ngasongwa alisema udhibiti huo unasaidia kuimarisha ushindani wa haki katika soko na kuongeza imani ya wawekezaji.

Aidha, ameeleza kuwa itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda ushindani wa haki katika soko na kumlinda mlaji ili kuhakikisha mazingira bora ya biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *