FAHAMU CHANZO CHA MENO KUFA GANZI, TIBA

MENO KUFA GANZI.

Tatizo la meno kufa ganzi kwa kitaalamu linaitwa Hypersensitivity, mara nyingi huwa linatokea hasa pale ambapo muhusika anatumia mswaki ambao kitaalamu hautakiwi kwa matumizi ya meno.

Mswaki huo ni ule wenye brashi ngumu ambao hupelekea kuondoa safu (layer) ya juu ya nje ya jino (enameli) na mara nyingi huwa inatokea hasa kwenye shingo ya jino, pale ambapo ufizi unaanzia.

Sehemu hii pamoja na safu ya ndani ya jino yaani dentine, ina vitundu vidogo dogo sana (stomata poles) ambavyo huruhusu upenyo wa kitu chochote chenye tindikali ,ubaridi ,pamoja na umoto kupenya kiurahisi na kusababisha hali ya ganzi.

Aidha, hali hii huwatokea watu ambao , wanapolala usiku huwa na tabia ya kutafuna meno na hivyo kuondoa ile lea ya juu ya jino (enamel) lakini pamoja na hayo pia huwatokea watu ambao meno yao yanakuwa wiki , hasa kutokana na ukosefu wa madini, calcium, fluoride.

SABABU.

Mvinyo: Mvinyo una kiwango kikubwa cha asidi ambayo huharibu sehemu ngumu ya nje ya jino inayoitwa enameli na kuacha matundu madogo kwenye meno yanayosababisha kuhifadhi vitu vinavyoweka rangi kwenye meno. Mfano; mvinyo mwekundu una chembechembe zinazoitwa ‘chromogens’ pamoja na ‘tannins’ ambavyo huweka rangi kwenye meno. Wanywaji wengi wa mvinyo hunywa taratibu kwa muda mrefu, hivyo kufanya tindikali (acid) iliyomo kwenye mvinyo kuharibu meno.

Pia tindikali hiyo husababisha kumomonyoka kwa enameli (dental erosion) na kuifanya kuwa dhaifu. Kama meno yako yameathirika kwa kuwa na rangi isiyokuridhisha na wakati mwingine kufa ganzi kutokana na kumomonyoka kwa enameli na unafikiri imetokana na matumizi ya mvinyo kama maelezo hapo juu, basi punguza matumizi haya na pata ushauri wa daktari wa kinywa na meno kutibu tatizo la ganzi.

Kutafuna kucha: Tabia hii inaweza kusababisha sehemu ya jino kusagika, kuwa dhaifu na hata kuvunjika. Pia na matatizo katika viungo vya taya na hivyo kuleta maumivu karibu na eneo la masikio (Temporomandibular joint dysfunction). Chanzo cha tabia hii kinaweza kuwa ni mazoea tu, au msongo wa mawazo na kazi.

Kusafisha meno kwa nguvu: Usitumie nguvu wakati wa kusafisha meno kwani unaweza kusababisha kuharibika kwa fizi zako na sehemu ya jino inayopakana na ufizi. Tumia mswaki wenye brashi laini na muda wa wastani wa dakika mbili, mara mbili kwa siku.

Matumizi ya meno kama kifaa: Tabia kama kufungua kizibo cha chupa, kufungua pakiti ngumu kama za maziwa kwa meno, kushika vitu kama sindano, kushikilia au kumenyea nyaya (kwa mafundi wa umeme, betri), kushikilia misumari (mafundi ujenzi) n.k. Kazi ya meno ni kutafuna chakula si kutumika kama kifaa mbadala.

Kutafuna vitu vigumu: Hii husababisha meno kusagika au kuweka nyufa na maumivu au ganzi kwa baadhi ya meno na hata kuvunjika kwa kipande cha jino. Tabia hii huanza taratibu kwa kuiga na baadae kuwa mazoea.

Matumizi ya vitu vyenye sukari mara kwa mara:  Kula kashata, ufuta, ubuyu, visheti, biskuti, pipi, keki, bazoka mara kwa mara, hasa vile vyenye sukari huongeza uwezekano wa kupata ugonjwa wa kuoza kwa meno. Mabaki ya vyakula hivi hutumiwa na bakteria (wanaoozesha meno) kutengeneza asidi inayoharibu sehemu ngumu ya nje ya jino na kuacha matundu.

Kahawa: Rangi ya kahawa huweka rangi kwenye enameli (sehemu ngumu ya nje ya jino) na asidi iliyopo ndani yake huweza kusababisha enameli kulika, hivyo rangi ya asili ya meno kupungua na kuanza kuwa na rangi ya njano.

Kutafuna kalamu: Tabia ya kutafuna penseli au kalamu inafanywa na watu wengi hasa wanapokuwa kwenye masomo, au kazi zinazohusisha kuandika na wakati mwingine msongo wa kazi nyingi. Tabia hii inaweza kusababisha meno kusagika kama itafanyika kwa muda mrefu. Kama unatabia hii ni vizuri ukatumia bazoka isiyo na sukari (sugarless gum), kila unapohitaji kutafuna kitu.

Sigara: Matumizi ya sigara na tumbaku za aina yoyote huweza kusababisha meno kubadilika rangi na kuongeza uwezekano wa kupata ugonjwa wa fizi. Pia matumizi ya tumbaku yanaweza kukusababishia saratani kwenye ulimi na mdomo. Tumia mbinu mbalimbali kukwepa na kuacha kabisa kuvuta sigara.

Kutafuna barafu: Kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya barafu na vinywaji baridi na vikali, baadhi ya watu hupendelea kutafuna barafu wakati wa kunywa vinywaji vyao. Kutafuna barafu kunaweza kusababisha meno kuvunjika, au kuweka nyufa zisizoonekana. Hii huweza kusababisha kupata maumivu au hali ya kufa ganzi wakati wa matumizi ya vitu vya baridi au vya moto.

Kusaga na kutafuna meno: Kusaga na kutafuna meno ni tabia inayohusisha msuguano wa meno unaotokea wakati wa usiku au hata mchana hivyo husababisha meno kusagika, kulika na kuweka nyufa ndogo ndogo kwenye sehemu ngumu ya jino na kuumwa kwa misuli ya uso na viungo vya taya. Pia meno huweza kupata ganzi mara kwa mara na kupata shida ya kutafuna.

Kutoga: Kutoga ulimi kunaweza kusababisha kuvuja kwa damu nyingi pale mshipa mkubwa wa damu utakapotobolewa. Pia kidonda kisipotunzwa vizuri huweza kupata maambukizi na kushindwa kupona kwa wakati. Kipini cha urembo kinachowekwa kwenye ulimi, mdomo au mashavu kinaweza kusababisha jino kuvunjika pale kiking’atwa kwa bahati mbaya– au kutengeneza nyufa ambazo zitakuwa zinauma na hata kusababisha ganzi kila unapokula kitu cha baridi, moto au hata hewa ya baridi ikiingia mdomoni.

Tembe za kulainisha koo: Tembe hizi mara nyingi huwekwa kiwango kikubwa cha sukari hivyo kukuongezea hatari ya kuoza kwa meno. Tabia ya matumizi ya chembe kama kiburudisho ni hatarishi kwa afya ya meno. Matumizi yasiyo sahihi, ni matumizi ya mara kwa mara yasiyohitajika. Tembe hizi zikitumika kwa muda mfupi hazina madhara yoyote kwenye meno.


Mirungi
: Hii hufanya meno kuwa na rangi isiyopendeza, meno hupoteza uimara wake na kutengeneza nyufa, mdomo kutoa harufu mbaya, huongeza uwezekanao wa kupata ugonjwa wa fizi na ina kilevi kinachosababisha uteja (addiction). Matumizi ya vitu hivi hujenga tabia ya mazoea (addiction) ambayo inahitaji ushauri nasaha na matibabu kutoka kwa madaktari wa saikolojia.

TIBA:

Mwone daktari akujuze kama kuna meno yaliyotoboka, huku ukizingatia namna ya upigaji mswaki hasa muda usiozidi dakika 15.

Daktari atafanya matibabu yameno yako kulingana na yalivyoathirika, halafu Daktari atakuelimisha ni dawa gani inafaa kwa meno yako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *